WANANCHI MANISPAA YA MOROGORO WASHAURIWA KUJENGA TABIA YA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA PAMOJA NA KUWA NA BIMA YA AFYA.
DIWANI wa Viti Maalum Manispaa ya Morogoro ,Mhe. Mwanaidi Ngurungu, amewashauri wananchi wa Manispaa ya Morogoro kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara kwa kufanya hivyo watatambua kama wana maradhi wataweza kupata huduma za matibabu kwa wakati.
Hayo ameyasema leo Oktoba 28/2022 katika hafla ya sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Kata ya Kingo yaliyofanyika katika Ofisi ya Kata.
Ngurungu, amesema kuwa utambuzi wa wazee uwe endelevu kwani kila mara wazee wanaongezeka hivyo wanapaswa kupewa huduma bora.
Aidha, ameshauri kwenye Hospitali, Vituo vya afya au Zahanati kuwepo na daktari maalum atakaye hudumia wazee ili wapate huduma nzuri.
Mwisho, amempongeza Diwani wa Kata ya Kingo, Mhe. Amini Tunda pamoja na Ofisi yake ya Kata na Baraza la Wazee la Kata kwa kuandaa vyema maadhimisho hayo huku akisema jukumu la kuwatunza wazee ni la kwetu sote na wazee wapate huduma sawa na watu wote.
Naye Diwani wa Kata ya Kingo, Mhe. Amini Tunda, amewataka Wananchi wa Kata hiyo kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili ziweze kuwasaidia kupata matibabu pindi watakapouguwa kwani maradhi huja muda wowote, wakati wowote na mahala popote bila ya kupiga hodi.
Upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Kingo, Amina Mamuya , ameushukuru Uongozi wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro kwa kushiriki maadhimisho hayo huku akiomba changamoto za wazee ziweze kutatuliwa ikiwamo huduma za upatikanaji wa dawa katika Vituo vya afya na posho za wajumbe wa baraza.
Katika maadhimisho hayo , huduma za kupima presha, sukari pamoja na lishe zilitolewa bure kupitia wataalamu wa afya kutoka Kituo cha Afya cha Uhuru ( Nunge) pamoja na elimu ya kujiunga na Mfuko wa Bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa.
Post a Comment