DC MSANDO AZINDUA MIONGOZO YA ELIMU MANISPAA YA MOROGORO, AITAKA MANISPAA KUJIKITA NA CHANGAMOTO ZA NDANI.
MKUU wa wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amezindua miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa elimu Manispaa ya Morogoro huku akiitaka Manispaa kujikita na changamoto za ndani zaidi.
Kauli hiyo ,ameitoa Septemba 29/2022 alipokuwa akizungunza na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari na viongozi wa Manispaa ya Morogoro kwenye uzinduzi wa miongozo hiyo eneo la Ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilakala.
DC Msando, amesema Manispaa ya Morogoro , hakuna sababu ya kutofanya vizuri katika suala la kitaaluma kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ikilinganisha na Halmashauri nyingine katika mkoa wa Morogoro.
Aidha, amesema kuwa , miongozo hiyo hususani wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu ya msingi ni mikakati ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji,usimamizi na ufuatiliaji na ushiriki wa wadau ili kufanikisha utekelezaji huo.
Hivyo,amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari kutumia miongozo ya usimamizi na uendeshaji iliyotolewa na serikali kufanya tathimini ya mara kwa mara ya hali ya elimu ili kurudisha heshima ya Manispaa ya Morogoro.
Ametoa agizo kuanza kuwafuatilia na kuwaandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza elimu ya awali na shule ya msingi ili waanze masomo ifikapo mwezi Januari 2023 na kusimamia watoto watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawe wameripoti mara shule zitakapofunguliwa.
Miongozo iliyozinduliwa katika Halmashauri hiyo,ni mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu ya msingi,uteuzi wa viongozi wa elimu katika mamlaka za serikali za mitaa na changamoto katika uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewahimiza walimu kuwa wabunifu, kujifunza ikiwamo kusoma vitabu mara kwa mara ili kupata maarifa na mbinu mpya zitakazowasaidia kufanya vizuri katika kazi zao za kila siku.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Chausiku Masegenya, wamejipanga kufanya vizuri katika sekta ya elimu ili watoto wote waliopo kwenye shule za msingi na sekondari wapate elimu bora na hatimaye waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Naye Afisa elimu sekondari Manispaa ya Morogoro, Gabriel Paul, amesema Manispaa ya Morogoro Shule za Sekondari za Serikali 27 na binafsi 28 .
Post a Comment