Header Ads

RC MWASSA ATANGAZA VITA KWA WAKANDARASI 'VISHOKA'.










MKUU  wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Abubakar Mwassa ametangaza vita dhidi ya wakandarasi wanaofanya kazi Mkoani humo wasiotekeleza kazi zao kwa ubora unaotakiwa ambao amewaita ‘vishoka’ huku akiwataka mara watakaposikia taarifa hizi waanze kufunga virago au kubadili utendaji wao wa kazi.

Fatma Mwassa ametoa agizo hilo kwa wakandarasi wa aina hiyo Oktoba 23 mwaka huu wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Hoteli ya Morena katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Amesema, ujenzi wa barabara nyingi ndani ya Mkoa huo zimejengwa chini ya kiwango na tatizo kubwa likiwa ni uwepo wa wakandarasi wengi wasiotekeleza kazi zao kwa ubora unaohitajika kwa mujibu wa mikataba wanayoisaini na kuagiza wakandarasi hao kutolipwa fedha wasipofanya kazi hizo kwa tija.

“sasa mimi nitangaze tu, nimetangaza vita na Wakandarasi vishoka, huko waliko taarifa hizi zikiwafikia waanze kufunga virago waondoke Morogoro, sababu hakuna Mkandarasi atakayelipwa bila kufanya kazi yenye tija”. amesema Fatma Mwassa.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amesikitishwa na ujenzi wa daraja lililojengwa Wilayani Kilombero likiwa chini ya kiwango na kuagiza daraja hilo kubomolewa haraka na kujengwa upya kabla yeye hajafika kulikagua vinginevyo mkandarasi anayehusika na ujenzi huo atachukuliwa hatua Kali za kisheria.

Wajumbe wa Kikao hicho wakiwa katika mjadara wa upatikanaji wa Maji hususan katika Manispaa ya Morogoro Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MORUWASA) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Tamimu Katakweba amesema hali ya upatikanaji wa maji katika Manispaa hiyo umefikia asilimia 48 chini ya lengo la Serikali la kufikisha upatikanaji wa Maji kwa asilimia 95 Mijini huku akitaja mikakati ya kufikia kuhakikisha asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.

Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa Manispaa hiyo inategemea maji kutokanBwawa la Mindu kama chanzo kikuu cha maji ambapo kwa Sasa uzalishaji wake ni lita milioni 35 hadi 37 kwa siku huku mahitaji yakiwa lita milioni 73.

Wakijadili suala la utunzaji mazingira na vyanzo vya maji, Wajumbe wa kikao hicho akiwemo Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Paramagamba Kabudi ameshauri Mkoa kuwa na Mkakati wa kuhifadhi mazingira kwa kuwa ni Mkoa pekee wenye vyanzo vingi vya Umeme unaotokana na Maji kwa asilimia zaidi ya tisini.

Amesema, Mkoa wa Morogoro unapitiwa na mito inayopeleka maji Bwawa la Mwalimu J. K. Nyerere na kuna vyanzo vya maji yanayokwenda Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam hivyo Mkoa unatakiwa kuwa na Mkakati maalum kwa ajili ya kulinda mazingira hususan kwenye vyanzo vya Maji ili bwawa la Mwalimu Nyerere liwe endelevu na Mikoa inayotegemea maji ambayo vyanzo vyake ni kutoka Morogoro iweze kupata maji yenye uhakika.

Aidha, wajumbe wa kikao hicho wameshauri zao la Mkonge kuongezwa na kuwa zao la Kimkoa baada ya mazao mawili ya Mpunga na Miwa kwa maana ya uzalishaji wa Sukari kwa kuwa hali ya hewa ya Mkoa huo na Ardhi vinaruhusu zao hilo kustawi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.