Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA MOROGORO AWATAKA WAZAZI KUWEKEZA KWENYE ELIMU.

               

Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, (katikati) akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi  Ujirani, Fred Fubile , Sola kwa ajili ya kuendelea kupata nishati katika Shue hiyo.(kulia) Afisa Elimu Msingi  Manispaa ya Morogoro, Chausiku Masegenya.(wapili kutoka kushoto) Afisa Utumishi Manispa a ya Morogoro , Pili Kitwana.

                  

                  

                 

                

               

                    
                   
                   
Madarasa mapya yanayoendelea na ujenzi.


MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewataka wazazi kuwekeza kwenye Elimu sambamba na kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Kauli hiyo, ameitoa leo Desemba 31/2020 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa na Ofisi ya Walimu Shule ya Msingi Ujirani Kataya Mkundi.

Lukuba,  amesema kuwa kuna hitajika nguvu za Wananchi na Serikali katika kuhakikisha watoto wote waliofaulu mtihani wanapata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.

Aidha, amechukua nafasi ya kuwaomba Waheshimiwa  Madiwani kufikisha ujumbe kwa wananchi ili wachangie nguvu zao kwa kujenga maboma na Serikali imalizie lengo ni kuwawezesha watoto wote waliofaulu mtihani kuendelea na masomo.

“Tupo hapa Shule ya Msingi Ujirani ambayo ipo umbali wa KM 18 kutoka Ofisi Kuu ya Manispaa, tumeona changamoto kama uhaba wa madawati, madarasa, matundu ya vyoo, shule kama hizi tunatakiwa kuziangalia kwa jicho la kipekee, mwenzetu alijitolea kujenga Shule hii lakini majengo yameshachoka toka 2004 hayana milango wala madirisha, lakini hata watoto wanaposoma madarasani haifurahishi ,tupo mjini na tunakaribia kuwa Jiji, niwaombe Wananchi wa Manispaa ya Morogoro jengeni maboma na sisi Serikali tumalizie ili watoto wetu wasome” Amesema Lukuba.

Hata hivyo, amemuagiza Afisa Elimu kwa kushirikiana na Mchumi wa Manispaa kupitia mapato ya ndani  kuhakikisha wanatenga  bajeti ya kutosha  ili waweze kukamilisha miundombinu.

Shule hiyo imetengewa kiasi cha fedha Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa pamoja na Ofisi ya Waalimu .

Katika hatua nyengine, Mkurugenzi ,amekabidhi Sola pamoja na betri vyenye  thamani ya shilingi milioni 1,500,000/= yenye uwezo wa kuwasha taa 10 na kuchaji simu ili iweze kutumika katika kusaidia Ofisi pamoja na waalimu wanaoishi shuleni hapo .

Mwisho,  amesema ukamilishaji wa maboma utaangalia sehemu ambapo wananchi watakapokuwa wameonyesha jitihada zao kwakukamilisha boma/maboma mapema na kuahidi Halmashauri kukamilisha maboma hayo haraka ili yaanze kutumika.

Naye, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, Chausiku Masegenya, amemshukuru Mkurugenzi kwa kuwa mstari wa mbele katika kuona changamoto za shule zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Masegenya, amewaomba Viongozi wenzake kuwa na moyo wa kusaidiana katika kutatua changamoto mbalimbali ili waweze kufikia malengo.

“Nampongeza sana Mkurugenzi kwa kazi nzuri ya kuwa mstari wa mbele katika kutatua kwa haraka changamoto za elimu, lakini nipende kutoa shukrani kwa  Waalimu kwa changamoto wanazokumbana nazo lakini kikubwa niwaombe Wakuu wa idara tuweze kufanya kazi kwa moyo wa kuwatumikia wananchi pamoja na kushirikiana kwani tukijafanya hivi hata kazi zetu tutakuwa tunazifanya kwa ufanisi wa hali ya juu” Amesema Masegenya.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ngerengere, Mwajuma Omary Mlimbo, amesema mtaa wake umekuwa na changamoto kubwa za shule mbili ambapo hadi sasa changamoto ambazo zimekuwa ni kero kubwa ni barabara kuwa mbaya  pamoja na pori linalozunguka barabara wanazopita wanafunzi.

Amesema uwepo wa pori umekuwa ni hatarishi kwa wanafunzi kwani vitendo vya ubakaji na uporwaji vimekuwa vikishamiri jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha kwa wananchi pamoja na wanafunzi.

Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ujirani, Mwl. Fred Fubile, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Afisa elimu pamoja na CMT kwa kutoa kiasi cha Shilingi  milioni 50 kwa ajili ya kupunguza changamoto za ukosefu wa vyumba vya madarasa kwani shule hiyo ilikuwa na madarasa 3 ambayo watoto wamekuwa wakisoma chumba kimoja madarasa 2.

 


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.