Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YATOA MKOPO WA PIKIPIKI ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 80 .

 



MANISPAA ya Morogoro imetoa Mkopo wa Pikipiki wenye thamani ya Shilingi Milioni 80 kwa vikundi viwili vya bodaboda ikiwamo Bomsate pamoja na Twaweza Mindu.

Ugawaji huo wa Pikipiki umefanyika katika eneo la Stendi mpya ya Daladala Mafiga Desemba 01/2020.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Albinus Mgonya,  amevitaka vikundi mbalimbali kufanya kazi kwa uweledi jambo ambalo litasaidia vikundi hivyo kufanya marejeshi ya fedha ili vikundi vingine venye uwitaji viweze kupata mkopo na kupiga hatua kimaendeleo.

Mhe. Mgonya amesema kuwa kama mikopo hiyo wataitumia kwa malengo yaliokusudiwa kwa muda mfupi wataweza kurejesha fedha kwa wakati na manispaa itaweza kuwapa mikopo mingine.

“Leo tunatoa mkopo wa Bodaboda wenye  thamani shilingi Milioni 80, tuvitumie vyombo hivi kwa malengo na turudishe fedha kwa wakati" Amesema Mgonya.

Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wanawawezesha kiuchumi watanzania ili wawe na maisha mazuri jambo ambalo litaleta tija, kwani wataweza kujiajiri wenyewe kupitia mkopo huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaaa ya Morogoro, Pili Kitwana, amesema kuwa vikundi hivyo vinatakiwa kurejesha fedha kwa wakati ili wengine waweze kufaidika na mikopo inayotolewa ndani ya Manispaa Morogoro.

Kitwana,amesema kuwa pikipiki walizotoa wamezikatia bima kubwa ili kuhakikisha vikundi hivyo wanafanya shughuli zao katika mazingira rafiki na kupata faida.

Amesema kuwa mpaka sasa vikundi vyote wamewapatia elimu ya kurejesha mikopo kwa wakati, huku akifafanua kuwa kama watazitunza vizuri wataweza kununua zakwao wenyewe baada ya miaka 5.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe,  amesema kuwa zoezi la kutoa mikopo ya bajaji na Pikipiki na sehemu ya kutimiza ndoto ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha kila mtanzania anakua na maisha mazuri.

Hata hivyo vikundi vilivyopata mikopo hiyo wameonekana kuwa na furaha huku wakiaidi kwenda kufanya kazi kwa ufanisi kwa ajili ya kupiga hatua za kimaendeleo.

Miongoni mwa vikundi vilivyopata mkopo ni pamoja na Mindu twaweza pikipiki 7 pamoja na Bomsate pikipiki 30 ambapo jumla ya pikipiki ni 37.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.