MADIWANI MANISPAA YA MOROGORO WATAKIWA KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO.
Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro baada wakiwa katika picha ya pamoja baaada ya kula kiapo katika uzinduzi wa Baraza Jipya leo.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Eng. Emmanuel Kalobelo, akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati wa kuzindua Baraza jipya la Madiwani Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, akihutubia Madiwani pamoja na Wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa Baraza Jipya la Madiwani.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood, akitoa salamu .
Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Christine Ishengoma akitoa salamu .
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma ,akitoa salamu za Chama .
KATIBU Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo, amewataka
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kubuni vyanzo vipya vya mapato
na kuboresha vyanzo vilivyopo ili kuwezesha Halmashauri kuweza kuongeza uwezo
wa kujitegemea kwa mapato ya ndani ya halmashauri.
Kalobelo, ameyasema leo wakati wa Uzinduzi wa Baraza la Madiwani
leo Desemba 14,2020 katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Stendi ya Mabasi Msavu.
Amesema kuwa Halmashauri ikiboresha mapato itasaidia halmashauri
kutoa huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo afya, elimu, Maji nk na
pia kiwango cha mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake itaongezeka.
Hata hivyo, amewataka Waheshimiwa Madiwani kutenga maeneo ya
uwekezaji kwa ajili ya viwanda vidogo, kati na vikubwa kufanya hivyo
kutaongeza Mapato ya halmashauri na Serikali
kuu.
Hata hivyo, amesema kuwa
ukusanyaji wa mapato ya ndani lazima uendane na nidhamu ya matumizi ya
fedha kwa hiyo ni jukumu la Baraza la Madiwani kusimamia na kuhakikisha
kuwa mapato yote yanayokusanywa katika vyanzo vya ndani yanatumika ipasavyo.
“”Nitoe rai kwa Manispaa kwamba hakikisheni fedha zinazokusanywa
kupitia katika miradi yote zisitumike zikiwa mbichi, bali zinatakiwa kupelekewa
benki na kutumika kwa kufuata utaratibu mzuri na uliosahohi kisheria lakini
fedha hizi za miradi ziende Benki kwa wakati, “ Amesema Eng. Kalobelo.
Katika hatua nyengine, amewataka Viongozi kuendelea kuhamasisha
Wananchi kujiunga na Bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa huku Serikali ikiwa na
kazi ya kuhakikisha kwamba Dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa uhakika ili
kuendelea kuboresha afya na Ustawi
wa Wananchi.
Ufuatiliaji wa mara kwa mara ufanyike ili kuhakikisha
miradi ya maendeleo inatekelezwa na lazima Waheshimiwa Madiwani utaratibu
wa kukagua miradi hiyo inayotekelezwa na Halmashauri kupitia kamati zako.
“ Nipongeze Baraza la Madiwani kwa kweli mmefanya vizuri sana
katika kipindi cha miaka 5 iliyopita , sasa tunataka uwepo wa Baraza Jipya uwe
chachu kubwa ya maendeleo, tutawapima baada ya miaka 5, yapo maendeleo
mmeyakuta, tunataka muyaendeleze na kuanzisha upya, lakini tusisahau
wafanyabiashara kuwajengea mazingira mazuri, lazima tuhakikishe kwamba
tunajenga kituo cha One Stop Centre kwa ajili ya wafanyabiashara wote”
Ameongeza Eng. Kalobelo.
Mwisho, amewataka Madiwani wahakikishe kwamba wanakamilisha
Ujenzi wa vyumba 26 vya Ujenzi wa Madarasa mapya na Madawati yake kabla ya mwezi Februari mwakani ili
Wanafunzi wapate kukaa na kusoma vizuri.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amewapongeza
Manispaa ya Morogoro kwa ufaulu wa Wanafunzi Kidato cha kwanza ambapo kwa Manispaa
Jumla ya Wanafunzi 7,577 wamefaulu kujiunga na Kidato cha kwanza.
Amesema kazi iliyopo mbeleni ni kuhakikisha wanatekeleza agizo
la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, la
kuhakikisha hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Februari , mwakani Wanafunzi wote
waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanaanza masomo wakiwa Madarasani
wakiwa wamekalia Madawati yao.
Msulwa, amesema darasa moja linajumla ya thamani ya Shilingi
Milioni 20, hivyo Manispaa itahitaji kutumia Shilingi Milioni 520 kujenga
madarasa mapya 26 bila kujumuisha ukamilishaji wa Maboma na samani zake.
“ Ndugu zangu , leo mmekula viapo na mmezindua Baraza jipya ,
katika agizo hili tuna siku 74, za kujenga Majengo 26 mapya na kumalizia maboma 13 ambapo madarasa hayo yanatakiwa
kukamilika na watoto wawe madarasani, hili ni agizo la Serikali ya CCM ambao
wote hapa ni Wanachama wake hivyo halina mjadala, niwasihi Waheshimiwa
Madiwani, tusianze vibaya kwa kushindwa kutekeleza agizo hili rasmi la Serikali
Kuu, kila siku lazima tulifanyie kazi , Mkurugenzi na Madiwani tusikae kimya
angalia kama kwenye Kata yako kuna Sekondari, licha ya fedha za Manispaa,
lakini tumeandaa utaratibu mzuri wa kukusanya michango kutoka kwa wadau wetu
mbalimbali wa maendeleo ili tuhakikishe zoezi hili , peke yetu hatuwezi , ni
lazima tushirikiane na Wadau wetu “ Amesema DC Msulwa.
“Nawaomba sana Waheshimiwa Madiwani tumpe ushirikiano Mkurugenzi
wa Manispaa yetu, katika kipindi kifupi nilichofanya naye kazi nimegundua kuwa
mkishikamana naye kasi yetu ya Maendeleo itaongezeka sana, mimi naamini mkitumia
uwezo wake na kujiepusha na migongano isiyo
na tija, Morogoro itaingia katika hadhi ya Jiji ikiwa mpya kabisa, Hongereni
sana Manispaa, chapeni kazi, “ Ameongeza DC Msulwa.
Kwa upande wa Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John, amewataka
madiwani hao kuwa na umoja na mshikamano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowasilishwa kwao
kutoka kwa wananchi ili kuweza kuzitatua na kuzijadili kwa pamoja.
Ruth, amewataka madiwani wa kata zote za
jimbo hilo kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta Maendeleo katika jimbo hilo
kwa kushirikiana vyema na Uongozi wa Manispaa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini,
Abdulaziz Abood, amesema atafanya kazi bila ubaguzi wowote hivyo ameomba
madiwani wote kumuunga mkono katika harakati za kuleta Maendeleo Jimbo la
Morogoro Mjini.
"Tufanye kazi kwa pamoja, mimi siko upande
wa mtu yeyote! Bali nahusiana na watu wote kikubwa ni kuleta Maendeleo ndani ya
Halmashauri yetu ya Manispaa ya Morogoro na tuvunje makundi kinachotakiwa ni
kwenda kuitekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM kwa vitendo kama tulivyo
ahidi kwa Wananchi " Amesema Mhe. Abood.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amehimiza umoja na mshikamano baina ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa
ya Morogoro ili kuweza kuwatumikia vyema
wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
Mhe.
Kihanga, amesema baada ya uchaguzi huo kumalizika viongozi wanajukumu na
wajibu wa kuwatumikia wananchi wao bila
kuchoka ili kuleta maendeleo yao na hatimaye kuweza kuchochea kasi ya ukuaji wa
uchumi.
Post a Comment