Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA MOROGORO AWATAKA WATENDAJI KATA KUHAKIKISHA MABOMA YA MADARASA YANAKAMILIKA KWA WAKATI ILI WANAFUNZI WALIOFAULU WAINGIE DARASANI .

                                           

Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akikagua ujenzi wa Madarasa Shule ya Sekondari Kihonda.

                                
                             
                                                                    
                       

MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ukamilishwaji wa Maboma yote ya Shule ikiwemo Msingi na Sekondari ili wanafunzi waliofaulu waingie darasani.

Kauli hiyo, ameitoa leo Desemba 21,2020 katika Shule ya Sekondari Kihonda  , wakati wa ziara ya kukagua Maboma yanayotakiwa kukamilishwa kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza waliofaulu.


Akizungumza na Waandishi wa habari, Lukuba, amesema kuwa huu sio wakati wa kuangalia pesa imeingia katika akaunti ya Kata au ya Shule kikubwa ni kasi ya ujenzi iongezwe ili madarasa yakamilike kwa wakati na Wanafunzi wasome wakiwa wamekaa katika madawati bila msongamano.

Lukuba, katika ziara hiyo amewasisitizia mafundi kwenda na kasi kubwa ili wanafunzi waanze kuyatumia madarasa hayo katika kupunguza msongamano darasani. 

‘’ifike wakati sisi jamii ndio tuwe wa kwanza kuanzisha miradi kisha ndio serikali iwekeze nguvu zake, nimekuja kuona maagizo ya Waziri Mkuu  yanatekelezwaje, lakini nitoe rai kwa Watendaji wote wa Kata kwa kushirikiana na , Watendaji wa Mitaa, kuwahimiza Wazazi na Wananchi kuongeza kasi ya uhamasishaji katika kufanikisha ujenzi wa Maboma , agizo hili ni la Serikali tunatakiwa kulifanyia kazi kwa haraka, Baada ya tamko la Mhe. Rais la elimu bure bila malipo Wazazi wamehamasika na kuwa na mwamko wa kusomesha Watoto  na Watoto wamefaulu hivyo ni wajibu wetu kuona Watoto hawa wote waliofaulu ifikapo Januari 11/ 2021 wanaingia darasani , wanafunzi wetu wana uhaba wa madarasa hatutaki mrundikano, tunataka yakamilike wanafunzi wasome katika mazingira ya kuachiana nafasi ili kuongeza kasi ya ufaulu, ukiwa katika mazingira mabaya hata ile hali ya ufundishaji inashuka, kazi nimeiona inaendelea lakini ongezeni kasi tumalize kazi mapema" Amesema Lukuba. 

Lukuba, amesema kuwa Jamii inaposhiriki ipasavyo kwa vitendo katika ujenzi wa miundo mbinu ya elimu huwa chachu ya kupata kilicho bora kabisa maana jamii huwa na uchungu nacho kutokana kuwekeza nguvu zao na huwa walinzi wakubwa. 


Mwisho ametoa wito kwa wananchi wote wa Manispaa ya Morogoro kuwa tayari kujitolea kwa hiari katika miradi ya maendeleo hususani katika Ujenzi wa Maboma ya Madarasa.

Shule ya Sekondari Kihonda ni miongoni mwa Shule iliyoingiziwa Shilingi Milioni 80, ambapo milioni 20 ni kwa ajili ya umaliziaji wa maboma 3 na shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa mapya 3 kwani inategemea kupokea jumla ya wanafunzi wa kidato cha kwanza  700 watakaojiunga na Shule.

Ikumbukwe kuwa Jumla ya Wanafunzi waliofanya mtihani Darasa la saba ni 8401, Wasichana 4336, Wavulana 4062 ambapo katika idadi hiyo jumla ya Wanafunzi 7577 walifaulu mitihani miongoni mwao wasichana 3927, wavulana 3650 sawa na asilimia 90.22% ya wanafunzi wote waliofaulu.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.