DIWANI KILAKALA AKABIDHI MIFUKO 10 YA SARUJI NA KUWATAKA WANANCHI KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO.
Diwani wa Kata ya Kilakala Mhe. Marco Kanga (wapili kutoka kulia) akikabidhi mifuko ya Saruji 10 kwa ajili ya ujenzi wa Kivuko kinachounganisha Mtaa wa Bong'ora na Mbogo .
Diwani wa Kilakala, akiwa na timu ya Viongozi wa Ngazi ya Mtaa wa Bong'ora mara baada ya makabidhianao ya Saruji.
Kivuko kinachoendelea na ujenzi kinachounganisha Mtaa wa Bong'ora na Mtaa wa Mbogo.
DIWANI wa Kata ya Kilakala, Marco Kanga, amewataka wananchi wa Kata ya Kilakala kuwa na desturi ya kuchangia na kujitolea nguvu kazi kwenye
ujenzi wa miradi ya kijamii hali itakayowafanya kupiga hatua kimaendeleo katika
maeneo yao.
Kauli hiyo
ameitoa leo Desemba 31/2020 wakati wa Ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya
maendeleo ikiwamo Ujenzi wa Kivuko kinachounganisha Mtaa wa Bong’ora na Mtaa wa
Mbogo Kata ya Kilakala pamoja na Ujenzi wa Vyumba 4 vya madarasa Shule ya Sekondari Mazoezi -Lupanga.
Kanga, amesema
kuwa viongozi wa ngazi zote kwa kushirikiana na wananchi
wanapaswa kushiriki katika kuchangia na kuhamasishana kuchangia maendeleo kwani
Diwani peke yake awezi kufanikisha mambo
yote katika Kata.
Aidha, amesema kuwa maendeleo hayana
chama, hivyo wananchi na viongozi wanapaswa kuwa wamoja kwa sababu watakao
tumia miradi hiyo ni watu wote bila kujali itikadi za kisiasa .
‘’katika maendeleo hatuangalii vyama,
kwa kuwa wanufaika wa miradi hii ni wananchi wa Kata yote ya Kilakala, Nampongeza
sana dada yangu Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilakala, Watendaji wa Mitaa pamoja
na Viongozi wa Serikali za Mitaa kwa namna
mlivyohamasisha wananchi kushiriki kuchangia ujenzi wa miradi mbali mbali
katika Kata yetu ikiwamo huu wa Kivuko ambapo zaidi ya Milioni moja 1,000,000/= wananchi wamechangia kufanikisha
hatua hii ya ujenzi iliyofikiwa” Amesema Kanga.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kanga, amekabidhi
jumla ya Mifuko 10 ya Saruji yenye thamani ya Shilingi 160,000/= kwa ajili ya ujenzi
wa Kivuko hicho kinachojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuweza kuwapatia
hamasa wananchi wake katika suala la uchangiaji wa maendeleo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa
Mtaa wa Bong’ora ,Yusta Medadi, amewataka Viongozi wa Mtaa wa Bong’ora kusimamia
ipasavyo ujenzi waKivuko hicho ili kutowavunja moyo wananchi walioshiriki katika
ujenzi huo.
“Tunamshukuru
sana Diwani wetu kwa kutupatia mifuko hii 10 ya Saruji kwa ajili ya kivuko
kinachounganisha Mtaa wa Bong’ora na Mbogo, kwakweli barabara ni changamoto ,
wananchi wamejitolea lakini tunamshukuru sana Mhe. Diwani kwani sio mchango
wake wa kwanza ameshachangia kiasi cha fedha hadi hatua hii tuliyofikia,
kikubwa amewaomba Viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Bong’ora kusimamia ipasavyo
ujenzi wa Kivuko hicho ili kutowavunja moyo wananchi walioshiriki katika ujenzi
huo” Amesema Medadi.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bong’ora , Bi Pokea Mrisho, ameshukuru kupata msaada wa Saruji huku akimtaka Diwani huyo kuendelea na moyo wa kujitolea kwa ajii ya maendeleo ya Wana Kilakala pamoja na wananchi wa Mtaa wa Bong’ora.
Kwa upande wa
Mwananchi wa Mtaa wa Bong’ora, Steven Konea, amewaomba Wadau na Viongozi kuongeza nguvu ya kuwasaidia
kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kivuko hicho na kivuko chengine pamoja na kuimarisha barabara hiyo kwani hata
udongo uliopo barabara hiyo unahitaji vifusi ili magari na malori yaweze kupita
vizuri.
Post a Comment