Header Ads

MHANDISI NYAMUHANGA APONGEZA MANISPAA YA MOROGORO KWA KUKAMILISHA UJENZI SOKO KUU LA KISASA.

 

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, (kushoto mwenye suti nyeusi ) , Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI , Mhandisi Joseph Nyamuhanga (katikati) pamoja na Watumishi ngazi ya Mkoa,  Wilaya na Manispaa wakiwa katika picha ya pamoja.

Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba (kulia) akiwa pamoja na Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI , Mhandisi Joseph Nyamuhanga (kushoto) , Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu (katikati) wakifurahia jambo wakati wa kutembelea mradi  wa Ujenzi wa Soko.

             
          
             
  







KATIBU Mkuu  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI , Mhandisi Joseph Nyamuhanga, ameonyesha kufurahishwa na ujenzi wa soko kuu la kisasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro katika ujenzi ambao umekamilika kwa asilimia 100 ambapo umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 17.6.


Pongezi hizo, zimetolewa leo Desemba 07/2020, baada ya Eng.Nyamuhanga kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa Soko Kuu la Kisasa pamoja na kupitia taarifa ya mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kuona maeneo mbalimbali katika soko hilo , Eng. Nyamuhanga, amesema kuwa licha ya kuwepo na ujenzi wa miradi ya masoko katika Mikoa ya Mtwara, Dodoma, Njombe na Dar es Salaam , lakini amefurahishwa na Ujenzi wa Soko la Manispaa ya Morogoro ambapo Ujenzi wake umezingatia mahitaji ya wafanyabiasha wanataka nini katika soko hilo.

 

"Nampongeza sana Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha hizi, lakini Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya , Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro na timu yake ya Wataalamu bila kumsa  Mhandisi aliyesimamia ujenzi huu,pamoja  na watumishi wote wa Manispaa ya Morogoro kwa ushirikiano mliouonyesha katika utekelezaji wa mradi huu ,hii inaonyesha jinsi gani mlivyo makini katika usimamizi wa miradi,Manispaa ya leo siyo jana angalia sasa mna stendi ya Msamvu,mmejenga stendi ya daladala,haya ni mafanikio makubwa sana katika Serikali ya awamu ya tano"Amesema Eng. Nyamuhanga.

 

 “Lengo la miradi hii ya Kimkakati ni kwa ajili ya kukuza Miji na kuzijengea Halmashauri uwezo wa kujitegemea, lakini nawapongeza sana tunakata matokeo chanya kama haya yaendane na thamani ya fedha zinazotolewa ."Ameongeza Eng. Nyamuhanga.


Eng. Nyamuhanga , amesema kufuatia ombi la Manispaa hiyo kutaka kutengeneza mitaro inayozunguka Soko, Ofisi ya TAMISEMI imepokea ombi hilo na wamekubali kutoa Shilingi Milioni 470 kwa jili ya kuanza mchakato wa ujenzi wa mitaro hiyo ili kuzuia maji kukaa wakati wa mvua.

“ Haiwezekani mradi mkubwa kama huu , ukazungukwa na maji wakati wa mvua, tumepokea maombi yenu , sasa tumekubali kuwapatia shilingi Milioni 470 , kwahiyo niwaombe TARURA Manispaa ya Morogoro waanze haraka sana mchakato wa kutangaza mdhabuni ili kazi hiyo ianze mara moja “ Ameongeza kwa msisitizo Eng. Nyamuhanga.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, ameipongeza Serikali kwa kuingiza Barabara ya Kisaki katika mpango wa kuweka lami ambapo itarahisisha usafirishaji wa mazao kutoka Morogoro Vijijini kuja Soko Kuu.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema Soko hilo linatarajia kutoa ajira 2500 kwa Wananchi, ambapo ajira rasmi 2000 na zisizo rasmi 500.

Lukuba, amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli, kwa kutoa fedha hizo kwani itasaidia sana Manispaa kupunguza kutegemea  ruzuku kutoka Serikali Kuu ambapo kwa mwaka wanategemea kukusanya fedha zaidi ya Bilioni 3 katika Soko hilo na kufanya ongezeko la Shilingi Bilioni 11 kutoka Bilioni 8 za Bajeti kwa mwaka.

Aidha, amesema Soko hilo linatarajia kufunguliwa rasmi Desemba 15, 2020.

 

Akieleze kuhusu mradi huo, Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu, amesema ujenzi  huo utakuwa na Maduka 304, Meza 900, maeneo makubwa 16 ya kupangishwa kwa mita za mraba (benki, maduka makubwa , ofisi nk) maegesho ya magari makubwa 5 ya mizigo kwa pamoja, maegesho ya magari madogo 143 kwa pamoja, vyoo, migahawa, stoo 36 za mitumba, bucha pamoja na eneo la kuchinjia kuku.


 

 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.