Header Ads

UVCCM WILAYA YA MOROGORO MJINI YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

Mwenyekiti UVCCM Wilaya ya Morogoro  Mjini, Ndg. Kudra Mdeng'o akiongoza maandamano ya Vijana.
Vijana wakijiandaa na maandamano.

JUMUIYA ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi CCM  Wilaya ya Morogoro Mjini, imeadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa maandamano ya Chipukizi wakiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM , Ndg. Kudra Mdeng'o pamoja na Katibu Hamasa wa Wilaya hiyo, Ndg. Jumanne Hussein.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Juni 15/2023 kwa kushirikisha Chipukizi wa Vijana pamoja na baadhi ya Viongozi wa Ngazi za Kata, Mdeng'o, amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuwakutanisha Vijana hao na kuwajengea upendo pamoja na kuwapa elimu juu ya ukatili wa kijinsia.

Mdeng'o, amesema kupitia maadhimisho hayo, Serikali na wadau wengine wanakumbushwa  kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi. 

Aidha, amesema kuwa maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.

Naye Katibu Hamasa Wilaya ya Morogoro Mjini, Jumanne Hussein, amesema siku ya leo wameitumia kama Vijana kukumbushana juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia.

Kauli mbiu ya mwaka huu  " ZINGATIA USALAMA WA MTOTO KATIKA ULIMWENGU WA KIDIJITALI yenye lengo la kuwataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya Mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Ikumbukwe kuwa Chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.

Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi. Kufuatia tukio hili, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.