Header Ads

DIWANI AKERWA NA MIKOPO YA KAUSHA DAMU


DIWANI wa Viti Maalum Manispaa ya Morogoro, Mhe. Aisha Kitime, amesema kitu kinachomuumiza ni kuona wakina mama wakiteseka na mikopo kandamizi ( kausha damu).

Kauli hiyo, ameitoa Juni 08/2023 ukumbi wa Mehayo Kata ya Mazimbu katika kikao chake na Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake UWT Kata ya Mazimbu katika ziara yake ya kutemebelea vikundi vya wanawake wa Jumuiya hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo wa wanavikundi, Mhe. Kitime, amesema mikopo ya kausha damu ina madhara makubwa hususani imekuwa ikigomabnisha ndoa pamoja na kurudisha nyuma maendeleo.

" Hii mikopo sio rafiki kwa familia zetu, inatuumiza sana wakina mama, ndoa zinavunjika kwa ajili ya hii mikopo, sasa tubadilike zipo taasisi za kifedha ambazo zimekuwa wakombozi wakubwa wa mikopo rahisi na yenye tija kwa kujiunga vikundi na kupata mikopo hiyo kuliko hii kandamizi" Amesema Mhe. Kitime.

Mhe. Kitime, amewataka wakina mama hao kufikisha taarifa kwa wenzao na kujiunga vikundi ili sasa waweze kupewa elimu ya mikopo na kuweza kupatiwa mikopo ambayo itakuwa na tija kwao.

Katika hatua nyengine, Mhe. Kitime, amegawa vitendea kazi kwa Matawi yote ya UWT Kata ya Mazimbu kwa ajili ya kurahisiha utendaji wao wa kazi huku akihidi kuendelea kuimarisha uhai wa Jumuiya hiyo.

Naye Katibu wa  UWT Kata ya Mazimbu,  Bahati Mwale, amemshukuru Mhe. Kitime na kumuahidi kuyatekeleza maelekezo aliyoyatoa kwa kushirikiana na wakina mama wenzake .

'" Tumeona dhamira ya Diwani wetu kwetu, sisi kama Jumuiya na vikundi vyetu hatutamuangusha, tunayabeba mawazo yake na kufikisha kwa wengine ili tutoke katika mikopo hii kandamizi twende katika mikopo yenye tija, lakini nimpongeze kwa kutupa vitendea kazi kwani sasa utaamsha hali ya kiutendaji katika jumuiya yetu ya UWT Kata " Amesema Mwale.

Ziara ya Mhe. Kitime ni ya siku mbili kutembelea wana vikundi ambapo Juni 08/2023 ameanza na vikundi vya Kata ya Lukobe, Mazimbu na Juni 09/2023 ataendelea na vikundi Kata ya Mafisa .

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.