Header Ads

RC MALIMA AIPONGEZA MANISPAA YA MOROGORO KUPATA HATI SAFI MWAKA WA FEDHA 2021/2022


MKUU wa Mkoa wa Morogoro , Mhe. Adam Malima, ameipongeza  Manispaa ya Morogoro  kwa kupata  hati safi kwa kipindi cha miaka nane (8)   mfululizo  kwenye  ukaguzi wa fedha mwaka 2021/2022.

Pongezi  hizo  amezitoa katika Kikao Maalum cha   Baraza la Madiwani la kujadili utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa juni 22/2023.

Akizungumza katika Mkutano huo, RC Malima, ameitaka Manispaa ya Morogoro  kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za Serikali CAG ili kuendelea kupata hati safi.

"Ninampongeza Mkurugenzi na watendaji wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana vyema na Baraza la Madiwani  kwa utendaji kazi mzuri ulioleta matokeo mazuri na kuiwezesha Halmashauri kupata hati safi kwa kipindi cha miaka nane , lakini niwaombe Madiwani  hii Manispaa ni yenu watendaji hawa ni wapita njia tu, tushikamane kuhakikisha tunaboresha huduma za jamii kama Ilani ya CCM inavyotaka chini ya Mwenyekiti wake ambaye ndiye Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan .”Amesema RC Malima.

Vilevile ameitaka Manispaa kusimamia vyanzo vya mapato vilivyopo ndani katika kuongeza mapato ya Halmashauri na sio kutegemea vyanzo vya nje.

Akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoa wa Morogoro, CPA, Peter Mwabwanga, amesema Manispaa ya Ubungo ilikuwa na hoja  68 ambapo kati hizo hoja 58 zilijibiwa vizuri na hoja 10 zimebakia  na hoja 6 mpya na hoja 4 za zamani.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma, amewataka watendaji na watumishi kuhakikisha kwamba wanawapatia  ushirikiano mzuri Madiwani wanapotaka kuongea na wananchi wao katika kutatua kero na changamoto za wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, ameipongeza  Manispaakwa  kupata hati safi, hati hiyo imekuja kutokana na ushirikiano baina ya  Baraza la Madiwani, Mkurugenzi, Wataalamu , Chama Cha Mapinduzi  CCM pamoja  Pamoja na watumishi kwa kufanya  kazi kwa kujituma na kufuata vigezo na malengo waliyojiwekea.

Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka watendaji kujitahidi kukusanya mapato pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kuweza kushughulikia changamoto za Wananchi.

Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro amesema kuwa haya ni  mafanikio makubwa sana kwa Manispaa , kwani kitendo cha kupata hati ya ukaguzi inayoridhisha kwa muda wa miaka nane mfululizo imetokana na utendaji kazi mzuri unaooneshwa na watumishi.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.