Header Ads

BARAZA LA WATOTO MANISPAA YA MOROGORO LAPATA VIONGOZI WAPYA .


BARAZA  la watoto  Manispaa ya Morogoro  lapata viongozi wapya katika uchaguzi uliofanyika Ukumbi wa  Ofisi ya Kata ya Mji Mkuu, juni 14/2023.

Katika uchaguzi huo, jumla ya wajumbe 11 walihudhuria na kuchagua viongozi kwa ngazi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti.

Katika matokeo hayo, Omary Fadhili kutoka shule ya Msingi Mafiga 'B'aliibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 7 na Fadhila Ally kutoka shule ya Sekondari Kola Hill alifanikiwa kupata nafasi ya Makamu mwenyekiti wa Baraza hilo kwa kupata kura 7.

Akizungumza katika uchaguzi  wa viongozi wa Baraza la Watoto, Afisa Ustawi Dawati la Watoto Manispaa ya Morogoro , Joyce Mugambi, amesema lengo la kuanzisha Baraza hilo ni  kupigania haki za watoto na kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto katika Halmashauri ambapo watoto hao wamejumuishwa na wanafunzi kutoka katika shule za Msingi na Sekondari.

Kuhusu nafasi ya Ukatibu, amesema watafanya uchaguzi huo lakini zaidi amewatakia majukumu mema Viongozi waliochaguliwa.

Kuhusu haki za Mtoto, Mugambi,  amewataka wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanazilinda na kuzihuisha tunu na haki za watoto. 

Aidha , Mugambi, amewataka Watoto kuripoti matukio yanayokiuka haki za watoto na kuzitolea haki za watoto kwa mlezi aliye karibu nawe na unayemwamini au kupiga simu namba 116 kupata msaada zaidi ili watoto waendelee kuwa katika mazingira huru na yenye furaha na amani kwa kupata haki za msingi. 

Hata hivyo,   amewataka Wazazi na Walezi kuimarisha upendo na umoja kwani familia ndio msingi Mkuu wa malezi ya Mtoto kwenye jamii na amewataka Watoto kuheshimiana,kupendana na kuthaminiana.

Sanjari na hapo, amechukua fursa ya kuwaalika wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16/2023 katika Viwanja vya shule ya Msingi Mwembesongo yatakayosindikizwa na maandamano yatakayoanza  saa 2:30 asubuhi shule ya Msingi Mtawala na kuelekea Mwembesongo Shule ya Msingi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi waliochaguliwa , wamesema watahakikisha kuwa wanatimiza wajibu wa kulitumikia Baraza la Watoto pamoja na kuhimiza upendo na mashikamano kwa watoto pamoja na kutoa taarifa juu ya matendo ya ukatili ambayo watoto wamekuwa wakifanyiwa.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.