RC MOROGORO AMSHUKURU RAIS SAMIA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA MKOANI HUMO.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiwa na viongozi mbalimbali wakati akikagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Gairo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akimpa pole mtoto Devoth Julius (5) anayepata matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Gairo baada ya kuumia Mguu wake akiendesha baiskeri.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima anawasikiliza kero ya upatikanaji hafifu wa maji kwa baadhi ya wanawake waliokuwa wanachota maji kwenye moja ya bomba Wilayani Gairo.
Moja ya mtambo wa kisasa wa kuchimbia kisima pamoja na mafundi wakiendelea na zoezi la uchimbaji wa visima katika eneo la Kisitwi Wilayani Gairo.
Picha mbalimbali za Wahe. Madiwani wakati wa Kikao.
Hapa Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye eneo ambalo uchimbaji wa visima unaendelea.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za Afya kwa Wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kwa kutoa fedha za kujenga vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya.
Mhe. Adam Malima ametoa pongezi hizo Juni 12 mwaka huu wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Gairo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kwa Halmashauri zote Tisa za Mkoa huo lakini pia kushiriki mabaraza ya Madiwani kwa ajili ya kusimamia kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG.
Akiwa katika Hospitali hiyo Mkuu wa Mkoa amefurahishwa na huduma zinazotolewa hospitalini hapo hivyo akawataka Wahe. Madiwani wa Halmashauri hiyo na nyingine kuwa mabalozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuyasema hayo mazuri yanayofanywa na Serikari ya awamu ya sita.
"...Dkt. Samia amepeleka x- Ray kama hizi na hapa nimezikuta kama hizo zinafanya kazi, unajua sio kiini macho...sasa haya ndo mambo ambayo Mwenyekiti wa Madiwani mnawajibika kuyasema, kweli kabisa..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Kwa sababu hiyo ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira Wilaya ya Gairo (GAUWASA) kuhakikisha wanakamilisha upatikanaji wa maji kwa wakazi hao ndani ya miezi mitatu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo ya kuchimba visima virefu na au kupata maji kwa njia ya mseleleko.
Sambamba na hayo Mhe. Adam Malima akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani aliitaka Halmashauri hiyo kukusanya mapato kwenye sekta ya mifugo kwani amesema Sekta hiyo inakusanya 6% tu makusanyo ya ndani kupitia ushuru wa machinjio na ushuru wa mifugo wakati Sekta ya kilimo inakusanya mapato kwa 34% hivyo kuitaka Sekta hiyo iwe na mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame amepongeza kasi ya Mkuu wa Mkoa katika utendaji kazi wake na kuahidi kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 wanakwemda kukusanya zaidi ya bilion moja ya mapato yasiyolindwa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Rachel Nyangasi amebainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili Halmashauri yao kuwa ni pamoja na upungufu wa vyombo vya usafiri jambo linalochangia kushuka kwa mapato na kuwa na miradi kutokamilika kwa wakati sababu ya ufuatiliaji mdogo unaosababishwa na uhaba wa vyombo vya usafiri.
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi - CCM tawi la Kisitwi Bw. Godson Ngunei amemuomba Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa chama na Serikali kuunga mkono juhudi za Wananchi waliochangia ujenzi wa nyumba ya mganga wa zahanati ya Kisitwi ili iweze kukamilika kwa wakati, aidha, Mwenyekiti huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa na viongozi alioambatana nao kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo.
Post a Comment