Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI, WANANCHI WATAKIWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU UTUNZAJI WA MAZINGIRA.


MANISPAA ya Morogoro kwa kushirikianana na wadau wa Mazingira, wameadhimisha siku ya Mazingira Duniani Juni 05/2023 kwa kufanya usafi katika eneo linalozunguka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na kupanda miti  ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha Jamii kujenga tabia ya usafi katika maeneo wanayoishi ama kufanyia shughuli zao mbalimbali.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Janeth Chatta, amesema kuwa  maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni kuhamasisha jamii duniani kote kuelewa masuala yahusuyo Mazingira na pia kuhamasisha watu wa jamii mbalimbali duniani kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira.

Chatta ,amesema kuwa siku hiyo imekuwa ukumbusho wa siku hiyo  kutoa fursa kwa jamii kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi katika Mazingira na kuhamasisha jamii kufanya mazingira yao kuwa salama na masafi katika maisha yeo na vizazi vyao.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga,  amesema Manispaa katika kuadhimisha siku hiyo ,imeona vyema kushirikiana na jamii kufanya usafi ikiwa ni njia moja wapo ya kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya usafi kwa kupenda mazingira yaliyo safi kwa usalama kwa afya zao.

Mhe. Kihanga, amesema wapo watu ambao hawafanyi usafi mpaka kusimamiwa na kuonya kuwa wahakikishe wanatii sheria bila shuruti kwani suala la uchafuzi wa Mazingira halina msamaha.

“Uchafu unaozalishwa na mtu mmoja huathiri watu zaidi ya mia moja kwani huweza kusababisha mlipuko wa magonjwa, hatuhitaji kubembelezana katika suala la mazingira wanaochafua mazingira wachukuliwe hatua za kisheria tunataka kuwa Jiji , hatuwezi kuwa Jiji kama bado mji wetu ni mchafu kila mmoja awajibike kuhakikisha Morogoro Manispaa inakuwa safi ” Amesema Mhe. Kihanga.

Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Mazingira Manispaa ya Morogoro, Mhe. Hamisi Kilongo, amesema sualala usafi wa mazingira ni  jukumu la kila mmoja na kuwataka wananchi kuendelea kutunza  mazingira yanayowazunguka  iwe ni nyumbani ama katika maeneo yao ya biashara.

Kwa upande wa Afisa Mazingira Manispaa ya Morogoro , Dauson Jeremia, amesema Manispaa ya Morogoro imekuwa ikifanya  shughuli ya usafi kila mwisho wa wiki (Jumamosi) ambapo wananchi katika makazi yao na maeneo ya biashara huwajibika kufanya usafi wa kina ambapo maeneo yote ya biashara hufungwa mpaka muda wa saa tatu asubuhi ndipo hufunguliwa baada ya usafi kukamilika.

Ikumbukwe kuwa Kila tarehe 5 Juni, kila mwaka Watanzania tunaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliamuliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972, wakati wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira huko Stockholm, nchini Sweden.

Azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nations Environment Programme (UNEP) lilipitishwa pia siku hiyo. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kila mwaka tarehe 5 Juni, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani mwaka 2023 " Tumia mifuko mbadala wa Plastiki; kwa ustawi wa Afya, Mazingira na Maendeleo ya Uchumi”.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.