MANYUKI YATWAA UBINGWA MASHINDANO YA POLISI JAMII KATA YA LUKOBE .
TIMU ya soka ya Manyuki Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro, imefanikiwa kuwa bingwa wa mashindano ya Polisi Jamii Kata ya Lukobe yaliyoandaliwa na Mkuu wa Kituo cha Lukobe Mkaguzi msaidizi wa Polisi Wilaya ya Morogoro ambaye ndiye Mkuu wa Kituo cha Kata ya lukobe kwa kushirikiana na Ofisi ya Kata ya Lukobe.
Akifunga mashindano hayo, mgeni rasmi wa mashindano hayo ambaye ndiye Diwani wa Kata ya Lukobe, Mhe. Selestine Mbilinyi, amesema lengo kuanzishwa Kombe hilo ilikuwa ni kutoa elimu na kuhamasisha jamii kushiriki kwenye ulinzi na usalama wa maisha yao na mali zao.
Mhe. Mbilinyi , amewataka vijana kupenda kushiriki michezo kwani ni ajira, uimarisha afya na ujenga ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Timu ya Manyuki imefanikiwa kutwaa ubingwa huo katika mchezo wa fainali wa mashindano hayo, baada ya kuibugiza timu ya Lukobe kwa mikwaju ya penati 4-3 na hivyo kunyakua zawadi ya pesa taslimu Shilingi 200,000/, Kombe na pamoja na mpira mmoja.
Timu ya Lukobe iliyoshika nafasi ya pili ya mashindano hayo imepata zawadi ya fedha taslmu shilingi 100000/= pamoja na mpira mmoja huku mshindi wa tatu Timu ya Tushikamane ikijinyakulia fedha taslmu shilingi 50000/=.
Naye Kamanda wa polisi Kamishina Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP . Hassan Maya amempongeza Polisi Kata ya Lukobe, pamoja na uongozi wa kata kwa namna walivyoshirikiana kuratibu na kufanikisha kufanyika mashindano hayo yenye lengo la kuwakutanisha vijana pamoja, kuwapa elimu ya Polisi Jamii ambayo itasaidia kuwaepusha na uhalifu.
ACP Maya, amesema kuwa mwisho wa mashindano haya ndiyo mwanzo wa maandalizi ya mashindano ya mwakani na kuahidi kuboresha na kuongeza zawadi zaidi kwa washindi wa mashindano hayo.
Aidha, ACP Maya, ametumia hadhira iliyofika kushuhudia fainali hiyo kuwataka wananchi wa kata ya Lukobe kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu kwa kumpa ushirikiano mkaguzi wa kata aliyepo.
Kwa upande wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kata ya Lukobe, ambaye ndiye muhusika Mkuu wa mashindano hayo, Zuena Mwita, amesema jumla ya timu 8 zilishiriki mashindano hayo ambayo yaliendeshwa kwa makundi hadi kufikia mchezo wa fainali.
Kamanda Mwita, amesema kuwa mashindano hayo yamepata mafanikio kwa kuwafikia watu wengi na kutoa elimu na hamasa iliyokusudiwa lakini imeweza pia kuendeleza michezo kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Lukobe.
Post a Comment