Header Ads

VIONGOZI CCM WATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA KUZINGATIA MAADILI,MIIKO NA MISINGI YAKE.


VIONGOZI na Wanachama wa  Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini  wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, miiko pamoja na misingi ya chama hicho sambamba na kufanya kazi kwa mashirikiano ili kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Ndg. Fikiri Juma, katika kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu CCM Wilaya ya Morogoro Mjini kilichofanyika Ukumbi wa Mbaraka Mwinshehe Manispaa ya Morogoro Juni 27/2023.

Fikiri, amesema kuwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wana jukumu la kuisimamia serikali katika kuhakikisha ilani ya CCM 2020/2025 inatekelezwa vyema na viongozi wanatekeleza miradi mbali mbali iliopo serikalini.

Aidha, amewataka Viongozi  wasisite kuitembelea na kuikaguwa miradi inayotekelezwa na serikali pamoja na kutoa maelekezo pale inapohitajika lengo likiwa ni kuhakikisha ahadi zilizotolewa na viongozi wakati  wakiinadi ilani hiyo zinatakelezwa kwa vitendo.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro , Solomon Kasaba, amewataka  viongozi wanaofanya kazi ya kuwasimamia wananchi kuepuka kupikiana majungu na kufitiniana na badala yake wafanye kazi kwa kushirikiana pamoja kwa kuwashirikisha vingozi wa serikali na Chama wakati wakitekeleza majukumu yao.

Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 , amesema muda wa uchaguzi bado na wale wanaotaka nafasi huu sio muda wake wawaache kwanza walioko mdarakani watimize wajibu wao muda ukifika Chama kinataratibu zake za uchaguzi.

Kasaba, ameagiza  viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi kufuata miongozo na taratibu za chama kwa kuacha tabia ya kupanga Safu kabla ya uchaguzi kwani kufanya hivyo kunasababisha kuibuka kwa makundi yasiokuwa na tija katika kukijenga chama.

Alionya kuwa, kwa mwanachama yoyote yule atakaebainika kukiuka misingi ya chama kwa kuanza kupanga safu mapema kabla ya uchaguzi basi uongozi wa Chama  hautasita kumchukulia hatua ikiwemo kulikata jina lake kwa nafasi alioiomba.

Aidha Masaba ,amesema  hali ya Usalama katika Mkoa wa Morogoro  imeimarika vizuri kutokana na mashirikiano mazuri yaliokuwepo baina ya viongozi wa Chama na serikali.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Twalib Belege, amesema Chama kimeshaanza zoezi la kuingiza wanachama katika mfumo wa Kielektroniki na kuwataka wanachama ambao hawajasajiliwa wasajiliwe.

Belege ,amesema zoezi hilo lililoanza Juni 26/2023 litafanyika kata 29 lakini utaratibu wake ni Kata moja kwa siku kuanzia nyumba kwa nyumba, shina kwa shina na tawi kwa tawi ili wanachama wote wanaosomeka katika reja waingie katika mfumo.

Mwisho Belege, ametoa wito kwa Jumuiya za Chama kubuni miradi itakayosaidia Jumuiya hizo kujijenga Kiuchumi ili ziweze kujitegemea kwa ajili ya kuimarisha uhai wa chama cha Mapinduzi.

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini ambaye pia ni Mjumbe, amesema  bajeti ya serikali iliopitishwa karibuni na Bunge inalenga kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili wananchi wake pamoja na kuwaletea maendeleo.

Kuhusu kero ya Maji, Mhe. Abood, amesema kuwa washafanya mazungumzo na Waziri wa Maji, Mhe. Aweso na muda wowote miradi ya maji itakamilika na wananchi kupata huduma hiyo waliyokuwa wakiisubiria kwa muda mrefu.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga  ambaye pia ni Mjumbe , amesema yapo mambo mengi ambayo Manispaa imefanya hususani katika ujenzi wa miradi ya maendeleo,kama vile Kituo cha afya Tungi na Lukobe , Ujenzi wa Zhanati mpya, Shule ya sekondari ya ghorofa Boma, Majengo ya utawala sekondari , ujenzi wa shule mpya za Sekondari Tubuyu, Lukobe na Mindu , n.k.

Kihanga, amesema kero za barabara zinakwenda kuisha kwani kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Manispaa ya Morogoro kwa makusanyo ya ndani inakwenda kununia Greda ambalo litatumika kuchonga barabara zote korofi na kurahisiha mawasiliano ya huduma ya usafiri.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.