MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA, WAZAZI WATAKIWA KUIMARISHA ULINZI KWA WATOTO
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wazazi kuwa walinzi wa watoto ili kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
Rai hiyo ameitoa Juni 16/2023 katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Manispaa ya Morogoro iliyofanyika viwanja vya shule ya Msingi Mwembesongo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Kihanga, amesema kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia pamoja na ukatili kwa watoto bado vinaongezeka miongoni mwa jamii kila siku.
"Siku ya leo tukiwa tunaadhimisha Mtoto wa Afrika ni wazi kuwa tunalenga kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa na kutekelezwa katika nyanja zote ili watoto waweze kuwa na ustawi mzuri na kufikia malengo na ndoto zao za kimaisha" Amesema Kihanga.
Kuna Aidha,Mhe. Kihanga, amewataka wazazi kuweka mazingira Salama dhidi ya matumizi ya vifaa vya kielektroniki vikiwemo simu, kompyuta, runinga, radio, na mitandao ya kijamii ikiwemo whats up, twitter na facebook wakati watoto wanapokuwa wanavitumia.
Kuhusu unyanyaswaji wa kijinsia, Mhe. Kihanga, amesema bado wanawake wengi wananyamaza wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia na sababu kubwa ni kutokuwa na elimu ya kutosha na hivyo ushindwa kuripoti.
Mwisho, Mh. Kihanga, amepongeza Bunge la watoto huku akisema , kazi kubwa ya Bunge la watoto ni kuendelea kutoa elimu kwa watoto na jamii ili kuwawezesha watoto na jamii kutetea haki za watoto na kuhamasisha utekelezaji na usimamizi wa haki hizo na kutoa taarifa sehemu husika pale zinapokiukwa.
Post a Comment