MAFIGA WAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA KWA KUZINDUA BARAZA LA WATOTO.
KATA ya Mafiga Manispaa ya Morogoro imeadhimisha kilele cha Siku ya Mtoto wa Afrika Duniani pamoja na kuzindua Baraza la Watoto la Kata hiyo.
Maadhimisho hayo yamefanyika Juni 14/2023 Mtaa wa CCM ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya siku hiyo ambayo Manispaa ya Morogoro itaadhimisha katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwembesongo Juni 16/2023.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro , Treiness Kadinda, amewataka wazazi kuwajali na kuwapenda watoto wao kwani waliwaleta duniani kwa mapenzi yao wenyewe yawapasa kuwalea na kuwakinga na ukatili wa kijinisia.
Kadinda , amesema kuwa, wazazi wanawajibika kikamilifu katika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu, kuwalinda na ukatili wa kijinsia pamoja na kupinga ndoa za utotoni ambazo zinawakatisha masomo watoto hao.
"Hakuna mtoto aliyeomba kuja duniani bali ni sisi wazazi kwa starehe zetu tumewaleta hawa watoto na lazima tuwajali na kuwalinda, kuwapa elimu na pia kutowakatisha masomo yao na kupelekea ndoa za utotoni," Amesema Kadinda.
Aidha, Kadinda, amewataka Watoto kuripoti matukio yanayokiuka haki za watoto na kuzitolea haki za watoto kwa mlezi aliye karibu nawe na unayemwamini au kupiga simu namba 116 kupata msaada zaidi ili watoto waendelee kuwa katika mazingira huru na yenye furaha na amani kwa kupata haki za msingi.
kwa upande wa Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, amesema kuwa watoto ni tunu ya taifa yapaswa kulindwa kwani kauli mbiu ya mwaka huu katika siku ya mtoto wa Afrika kwa hapa nchini inayosema " ZINGATIA USALAMA WA MTOTO KATIKA ULIMWENGU WA KIDIJITALI" inalenga katika kuhamasisha ulinzi wa watoto kwani watoto wamekuwa wakijiingiza katika mitandao ya kijamii na kuiga tamaduni ambazo sio aili ya mwafrika.
Afisa Lishe Manispaa ya Morogoro, Jacqueline Mashurano,amewataka wazazi kuwapatia watoto matone ya vitamini A pamoja na dawa za minyoo.
Mashurano, amewataka wazazi kuzingatia lishe bora kwa watoto ili wawe na afya bora.
Aidha, ameshauri shuleni kuanzishwa klabu za lishe kwa ajili ya watoto kupewa elimu bora ya lishe katika kutokomeza hali ya udumavu kwa watoto.
Mtendaji Kata ya Mafiga , Amina Saidi, amewataka Wazazi na Walezi kuimarisha upendo na umoja kwani familia ndio msingi Mkuu wa malezi ya Mtoto kwenye jamii na kuwataka Watoto kuheshimiana,kupendana na kuthaminiana.
Katika hatua nyingine, Kata ya Mafiga iliweza kuzindua Baraza la Watoto ambapo mgeni rasmi wa maadhimisho hayo aliweza kuzindua Baraza hilo.
Maadhimisho haya yalienda sambamba utoaji wa elimu ya lishe na watoa huduma wa lishe ngazi ya Kata waliweza kugawa uji kwa watoto ambao umechanganywa na mchanganyiko wa lishe mbalimbali.
Post a Comment