Header Ads

RC MALIMA AUNDA KAMATI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA HALMASHAURI.



Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima meunda kamati  maalum itakayo husika kutoa ushauri kwa Halmashauri za Mkoa huo ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuhusu makusanyo ya  ndani ili kufikia malengo halisi.

Mhe. Malima ameyasema hayo Juni 20 mwaka huu wakati wa kikao cha Baraza maalum la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kilichohusu kujibu Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG za mwaka 2021/2022.

Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri nne kati halmashauri tisa za Mkoa huo ambazo zinachangamoto kubwa katika ukusanyaji wa mapato na matumizi yake, na kwamba anaunda timu  itakayopitia taarifa za mapato ya Halmashauri hizo na kufanya tathmini ya taarifa hizo kisha kutoa ushauri wa namna ya kuboresha.

"...yapo mengi ya kusema kwenye Halmashauri yenu, nimeteua tume ya uchumi....kwa hiyo hawa mabwana watapita kwenye halmashauri yenu wajadiliane swali moja hadi jingine haswa hili la makadirio..." amesema Mhe. Adam Malima.

Aidha, amewaagiza Wahe. Madiwani kuwa na timu ya kusimamia miradi ya maendeleo katika Halmashauri yao angalau madiwani watatu kwa kila mradi mmoja, kwa kufanya hivyo amesema kutaongeza chachu ya ubora kwenye miradi husika na kukamilika kwa wakati.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo watakao shindwa kwenda na kasi yake katika utendaji  kazi wao kuachia nafasi hizo kabla yeye hajawachukulia hatua.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya mipango na uratibu Bw. Anza Ameni Ndosa kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, ameisisitiza Halmashauri hiyo kusimamia miradi ya Afya, elimu na maji kwa kuwashirikisha Wahe. Madiwani ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na ubora unaohitajika.

Naye, Mkaguzi wa nje na mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Morogoro CPA Peter Mwabwanga amesema katika  kipindi cha miaka mitatu 2019 hadi 2021 wanafunzi wanne kati ya kumi wa Sekondari wa Halmashauri hiyo waliacha shule, na kuwataka kuweka mikakati mahsusi ya kuhakikisha wanadhibiti suala hilo.

Baada ya majadiliano ya kina Mkuu wa Mkoa ameagiza kiwepo kikao kingine cha baraza la madiwani ambacho kitafanyika mwezi Julai mwaka huu huku akiwataka wajumbe wa menejimenti ya Halmashauri hiyo  kuja na hoja na majibu yanayojitosheleza.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.