DIWANI BUTABILE AITAKA UWT MAFIGA KUWA NA MIKAKATI YA KUJIIMARISHA KUCHUMI.
DIWANI wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, ameutaka Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Mafiga kujipanga upya kimkakati katika kujiimarisha kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kutimiza malengo, dira na shabaha ya jumuiya hiyo, katika kutataua changamoto za wanawake katika Kata hiyo sambamba na kuwafungamanisha katika kutumia fursa za kujikwamua na umasikini na kujiletea maendeleo endelevu.
Hayo ameyasema Juni 30/2023 katika Kikao cha Baraza la Kawaida la UWT Kata ya Mafiga.
Butabile, amesema kuwa kumekuwa na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali za kuwaletea maendeleao wananchi katika nyanja za uimarishaji wa huduma mbali mbali za kijamii ikiwemo Maji safi na salama, Afya, Kilimo, ujenzi wa miundombinu ya kisasa pamoja na kuimarisha huduma za nishati ya umeme maeneo ambayo yanampa unafuu mkubwa mwanamke ili kuweza kufanya shughuli za maendeleo,
Aidha, amewataka viongozi waliochaguliwa kuwa kiungo kizuri baina yao na serikali hasa katika ufuatiliaji wa miradi hiyo ambayo inaligusa kundi kubwa la wanawake katika jamii.
“Wanawake katika historia ya Taifa letu waliunganisha watu wa rika zote na hadhi tofauti katika harakati za kudai uhuru, dhima hii ya kuwaunganisha watu ni yetu sisi wanawake, hatuwezi kuikimbia kama vile ambavyo hatuwezi kukimbia na kuziona familia zetu zikisambaratika. Mwanamke ni muhimili mkuu katika kuunganisha familia na jamii na vivyo hivyo ni lazima tubebe jukumu la kuunganisha, ili Chama chetu kiendelee kuwa madhubuti siku hadi siku” Alisema.
Katika hatua nyengine, Mhe. Butabile, ametoa wito kwa viongozi hususani wanawake kubeba ajenda ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia na watoto kwenye vikao vyote kuanzia kwenye maeneo yao.
" Niendelee kuiomba UWT , udhalilishaji wa kijinsia upo, nawakumbusha kuendelea kupaza sauti zenu katika kupinga aina zote za udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, niombe hili lianze kwa ngazi zote kuanzia shina hadi Kata ili kuondokana na vitendo hivyo na ni vyema kushirikiana pamoja katika kupiga vita kwa lengo la kupunguza maumivu na kuongeza furaha katika jamii" Amesema Butabile.
Aidha,Butabile, ameitaka UWT Kata ya Mafiga kuendelea kujipanga vyema katika kuimarisha jumuiya hiyo kiuchumi kwa kuwa na miradi ya uwekezaji yenye kwenda na wakati na kuisimamia vyema ili kuleta tija kwa taasisi hiyo ambayo ndio tegemeo kubwa katika ukombozi wa wanawake nchini kisiasa.
"Kama mnavyojua uwezo wa kiuchumi hununua uwezo wa siasa, hivyo tusiposimama vizuri na kwa sababu hatuna nguvu ya kiuchumi huenda tukanunuliwa kisiasa, twendeni kukajiimarishe na tukajipange vizuri ili kufikia lengo” Ameongeza Butabile.
Hata hivyo,Mhe. Butabile amezipongeza jumuiya za Chama Cha Mapinduzi Kata ya Mafiga (WAZAZI, UVCCM na UWT) kwa kukamilisha chaguzi katika ngazi zote ambapo amezikumbusha kuwa jukumu kubwa liliko mbeleni ni kusimama na serikali katika kufanya shughuli za kujiletea maendeleo bila kujali itikadi za kisiasa na kwa kutanguliza Utanzania jambo ambalo litaendeleza ushirikiano, umoja na mshikamano.
Kwa upande wa Katibu wa CCM Kata ya Mafiga,Bi. Farida Rajabu, amewahimiza viongozi wa Jumuiya zote za Kata kuhakikisha wanaweka mikakati kwenye jamii namna ya kupambana kutokomeza ukatili na malezi duni yanayochangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili huku akibainisha kuwa yanaleta athari za kimwili, kisaikolojia na kiuchumi.
Bi. Farida, amesema wanawake Viongozi wana nafasi ya kuzungumzia ajenda ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwani, pamoja na takwimu kuonesha wanawake wanafanyiwa ukatili, kuna baadhi ya wanawake wanakatili watoto au wanakatili wengine au wanajikatili wenyewe.
Naye Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mafiga, Thabitha Justo, amesema ushauri waliotoa viongozi watauzingatia na katika vikao vyao kuanzia ngazi za Matawi watajikita katika kujadili mambo yenye kuongeza msukumo wa kuleta maendeleo katika jamii kwa kujadili kwa kina changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake wa Kata hiyo hususani kupiga vita dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Post a Comment