Header Ads

TIC YATEKELEZA AGIZO LA RAIS JPM YAKAMILISHA TARATIBU ZA UWEKEZAJI KIWANDA CHA VIFAA VYA UMEME KIGAMBONI


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi, (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki wa kampuni ya uzalishaji wa vifaa vya umeme kutoka Misri  iitwayo Elsewedy, Ibrahim Qamar (kulia) wakati alipoenda kutembelea maendeleo ya uwekezaji wa kiwanda hicho kilichopo Kigamboni- Dar es Salaam, katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania, Tanesco, Dkt Tito Mwinuka.   

 Mkurugenzi wa  Kampuni ya uzalishaji wa vifaa vya umeme Ukanda wa Afrika Mashariki kutoka Misri  iitwayo Elsewedy, Ibrahim Qamar (kushoto), akizungumza na wanahabari pamoja na Maofisa  kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC pamoja na Uongozi kutoka Shirika la Umeme Tanzania Tanecso, wakati wa ziara ya ya kikazi ya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Dkt. Maduhu Kazi alipoenda kutembelea maendeleo ya uwekezaji wa kiwanda hicho kilichopo Kigamboni- Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi (wapili kushoto), akipata ufafanuzi wa ramani ya ujenzi wa kiwanda hicho jinsi kitakavyokuwa pindi kitakapokamilika kutoka kwa Mkurugenzi wa kiwanda hicho Abdelfattah Elattar (kushoto) wakati alipoenda kutembelea maendeleo ya uwekezaji wa kiwanda cha uzalishaji wa umeme  kilichopo Kigamboni- Dar es Salaam.

KUTOKANA na agizo la Rais John Magufuli kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) lililokitaka kituo hicho kumsaidia mwekezaji kutoka Misri. Tayari kampuni hiyo ya utengenezaji wa vifaa vya umeme  imeanza ujenzi wa kiwanda chake nchini kwa gharama ya Sh bilioni 100.

Itazalisha transfoma, nyanya za umeme na vipuli vingine vinavyohitajika kwenye umeme.

Kampuni hiyo ilikabiliwa na changamoto kadhaa za uwekezaji ambapo Julai 16 mwaka jana Rais John Magufuli wakati wa uapishwaji wa Mkurugenzi mpya wa kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk Maduhu Kazi, alimwagiza Mkurugenzi huyo kati ya mambo mengine atatue changamoto za mwekezaji huyo.

Miezi sita tangu kuapishwa kwake, Jana Mkurugenzi Mkuu wa TIC, Dk Maduhu Kazi akiongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco) Dk Tito Mwinuka na watendaji wengine wa TIC walitembelea uwekezaji wa kiwanda hicho, Kigamboni.

Kiwanda hicho chenye ukubwa wa Kilomita za Mraba 120,000 kina uwezo wa kuzalisha nyaya za umeme tani 15,000 kwa mwezi, Mashine za kupozea umeme(transfoma) 400 kwa mwezi na bidhaa nyingine muhimu zinazohitajika kwenye uzalishaji wa umeme.

Akizungumzia kwa undani kuhusiana na kiwanda hicho, Mkurugenzi wa Kampuni ya Elsewedy Ukanda wa Afrika Mashariki, Ibrahim Qamar alisema kuwa uwekezaji huo umetokana na sera nzuri za uwekezaji zilizopo hapa nchini ambazo ziliivutia kampuni hiyo kuwekeza tangu awali.

Alisema kuwa licha ya kutokea kwa changamoto zilizosababisha kutaka kuondoka, lakini serikali ya Rais Magufuli iliingia kati huku na wamerejea na kuahidi kuongeza uwekezaji wa nchini huku akisifia ushirikiano anaoendelea kuupata kutoka TIC.

Alisema TIC imesaidia kwa kiasi kikubwa kuishawishi Bodi ya kampuni hiyo kuichagua Tanzania kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji wa bidhaa hizo za umeme kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.

Alisema, kiwanda hicho kitazalisha bidhaa za umeme kwa nchi za Afrika Mashariki na baadae Afrika nzima na pia kitajenga Chuo cha Ufundi umeme kwa ajili ya kuwanoa wafanyakazi watakaoajiliwa kiwandani hapo.

Alisema kiwanda kitaajili wafanyakazi zaidi ya 400 ambapo kitaanza na wafanyakazi 250 kisha kuongeza wengine zaidi hadi kufikia 400.

Alisema, watakaoajiliwa watakuwa ni sehemu ya utekelezwaji wa nia ya kuitangaza Tanzania kimataifa katika uzalishaji umeme ndiyo maana chuo hicho kimeanzishwa kuwajengea uwezo zaidi.

Katika kufanikisha uwekezaji bora zaidi na weney tija, kiwanda hicho kitatumia mfumo wa roboti kuzalisha vifaa hivyo huku lengo likiwa ni kuzalisha bidhaa bora zaidi za kisasa na kwa sasa kimeshaagiza mashine hizo zinazotarajiwa kuingia nchini kuanzia mwezi wa nne.

Alisema,:Kwa sasa kazi inayoendelea ni kuanza ujenzi wa kiwanda ambapo msingi umeshachimbwa na shughuli za kuanza kunyanyua kuta zinaendelea,

Lakini wakati hata yakiendelea tumeshaagiza mashine za kutengenezea bidhaa hizo za umeme tunataka Tanzania iwe ndio nchi ya kuzalisha bidhaa za umeme kwa Afrika Mashariki na Kati na Afrika nzima’’.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa (TIC), Dk Maduhu Kazi aliwataka wawekezaji wengine kujitokeza kwa wingi huku akibainisha kuwa serikali kupitia kituo hicho imejipanga kuwawezesha kufanikisha uwekezaji wao kwa haraka.

Alisema kiwanda hicho cha Elsewedy kitatoa ajira kwa watanzania na kuchangia pato la taifa hatua ambayo ni utekelezwaji wa sera ya viwanda ya serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli.

Alibainisha kuwa bidhaa nyingi ambazo awali zilikuwa zikinunuliwa nje ya nchi na kuigharimu nchi mabilioni ya fedha kwa sasa zinazalishwa nchini na kuharakisha maendeleo.

Alisema Tanzania ina fursa nyingi zaidi za uwekezaji

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Tito Mwinuka alibainisha kuwa uwekezaji huo utafanikisha miradi  mbalimbali ya umeme kwa ufanisi na kwa gharama nafuu kwa kuwa bidhaa kwa wingi zitakuwa zikipatikana hapa nchini.

Alisema kwa kampuni ambazo zimeshaanza kuzalisha hapa nchini bidhaa za umeme, zimesaidia kwa kiasi kikubwa kurahisha upatikanaji wa umeme.

 

 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.