Header Ads

MAGUFULI AWATAKA WAFANYABIASHARA SOKO KUU KINGALU KUCHAPA KAZI, WAKATI KERO ZAO ZIKISHUGHULIKIWA.

 

       

     












     

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, amewataka  Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kingalu Manispaa ya Morogoro kuendelea kufanya kazi wakati kero na changamoto zao zikiendelea kushughulikiwa.

Hayo ameyazungumza Februari 11/2021, wakati akizindua Soko hilo ambalo limegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 17.6.

Akizungumza na Waandishi wa habari maada baada ya kuzindua Soko hilo,amesema Jumla ya Shilingi Bilioni 361 fedha za Serikali zimetumika katika ujenzi wa Masoko ya kisasa 22 ambapo mpaka sasa ni masoko 9 ambayo yameshakamilika mengine yakiwa katika hatua za kukamilika.

Magufuli, amesema kuwa, katika Masoko yote , Soko la Kingalu Manispaa ya Morogoro ni la kwanza likiwa limetumia Bilioni 17.6, likifuatiwa na Soko la Ndugai Dododoma  Bilioni 14.6 na la tatu Soko la Kisutu Ilala Bilioni 13.4.

Hata hivyo baada ya kutembelea wafanyabiashara wa Soko hilo amekumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya watu kupangishiwa na madalali kwa kiwango kikubwa cha fedha pamoja na tozo ya ushuru kwa mizigo inayoingia Sokoni.

“Nimepita kwa Wafanyabiashara , kero zao zimenigusa sana, niombe Uongozi wa Mkoa wa Morogoro hizi changamoto zihakikishe zinapatiwa ufumbuzi haraka baada ya kuondoka, namuagiza Waziri Jaffo shughulikia haya mapema, na hakuna mfanyabiashara ambaye mzigo wake upo chini ya tani moja kutozwa ushuru” Amesema Magufuli.

“Niwaombe wafanyabiashara nyinyi ni wazalendo, fanyeni kazi yale mliyoniambia nimewaachia viongozi wangu washughulike nayo, tunataka kuona mkifanya biashara zenu kwa haki bila kunyanyaswa, lakini pia mpendane, suala la mizigo yenu hamtalipa ushuru , mtakacholipa ni bei ya maeneo ambayo mmepangishwa tu lakini huu ushuru ambao Serikali ilishatoa maelekezo usitishwe haraka, Serikali yangu ipo kwa ajili ya wanyonge , fanyeni kazi msivunje sheria” meongeza Magufuli.

Katika hatua nyengine, ameomba Viwanda vilivyokufa viendelee kufufuliwa na vifanye kazi ili vizalishe ajira kwa wananchi na kuiongezea taifa pato katika kufikia uchumi wa Viwanda.

Hata hivyo, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Morogoro, Mhe. Abdulaziz Abood kwa uchapakazi wake huku akisema ataendelea kushirikiana vyema na Wana Morogoro husuani katika kuboresha huduma ya afya na miundombinu ili kuweza kutumika kujenga uchumi wa Taifa pamoja na Mkoa wa Morogoro ikiwa ni utekelezaji Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Lakini amewataka wale wote ambao wamekuwa wakishiriki katika tozo kubwa za Vizimba kuwapangishia wengine walipe fedha hizo mara moja kwani Soko hilo limejengwa na fedha za Serikali na sio kwa ajili ya kuwanufaisha watu.

Mwisho, amewashukuru Wananchi wa Mkoa wa Morogoro kwa kuonesha mapenzi memea ya kumpa kura nyingi za ndio katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020 na kufanya Morogoro kuongoza kura asilimia 96 kwa mikoa yote Tanzania kwa kura nyingi za rahisi ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro iliongoza kwa kura kwa asilimia 99.6  kuliko Halmashauri zote nchini .

Waziri wa TAMISEM, Mhe. Selemani Jaffo, amesema Soko hilo baada ya kukamilika litakuwa na manufaa makubwa ya kuweza kuibadilisha Manispaa ya Morogoro pamoja na ustawi wa maisha yao.

Jaffo, amesema Soko la Morogoro ni miongoni mwa Masoko 22 ambayo yametekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Aidha, amewataka Viongozi wa Morogoro kuhakikisha wanaliendesha Soko hilo vizuri ili wananchi waweze kupata fursa nzuri ya maendeleo.

K wa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, amemshukuru Rais kwa kutembelea Mkoa wa Morogoro na kumpongeza kwa ushindi alioupata wa kishindi huku akisema kuwa  ushindi wa Mhe. Rais umetokana na kazi alizozifanya katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.

Sanare, amemshukuru Mhe. Rais kwa ujenzi wa miradi mikubwa katika mkoa wa Morogoro ikiwamo mradi wa SGR, Bwawa la Umeme, Stendi ya Msamvu, Stendi ya Daladala Mafiga , Soko Kuu la kisasa pamoja na kuboresha huduma za afya kwa kujenga  Hospitali za Wilaya,Vituo vya afya na miundombinu.

“Mh. Rais umetupa heshima kubwa ya kutupatia miradi mikubwa, tunaamini miradi hii ikikamilika itafanya maendeleo yaende kwa kasi kubwa , tuna miradi  mbali mbali ya kimkakati kama Soko hili, umetupa fedha nyingi za kujenga  Hospitali pamoja na vituo vya afya 17 , Ujenzi wa madarasa 257 na sasa asilimia 87% tumamliza na Vijana wote wote wamejiunga na  shule na tunatarajia ifikapo tarehe 20/2/2021 wale wachache wote wawe wameingia darasani, miradi ya maji , miundombinu , lakini changamoto ya ukubwa wa Wilaya zetu ambapo tunaomba uangalie jinsi ya kuzigawa maana ni kubwa sana na kuna muda wananchi wengine wanashindwa kufikiwa, tunajua haya yote umefanya kwa mapenzi yako ya kutaka kuona mkoa wetu unakuwa kiuchumi, tunakuomba

Naye Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood, amemshukuru Mhe. Rais kwa kuipatia Manispaa ya Morogoro Bilioni 17.6 kwa ajili ya ujenzi wa Soko hilo.

Mhe. Azizi, amesema kuwa Soko ni zuri na Wananchi wa Morogoro wamelipenda na kuanza kunufaika nalo licha ya kuwa na changamoto.

Aidha, amesema  licha ya Soko hilo kuwa zuri lakini zipo changamoto nyingi ikiwamo kuzuia Bajaji, bodaboda na daladala kuingia kushusha Wateja ndani.

Mbali na hayo, Mhe. Abood amemshukuru Mhe. Rais ,kwa kuipatia Manispaa ya Morogoro fedha kwa ajili ya kutekeleza  miradi mikubwa  ikiwamo mradi wa Stendi Mpya ya Daladala mafiga, mradi wa maji wenye thamani ya shilingi Bilioni 185, mradi wa maji Kihonda na Lukobe   ambao utagharimu shilingi Bilioni 2.2 ambapo mpaka sasa zimeshatoka shilingi milioni 100 ambapo kwa sasa fedha zilizobakia ni Bilioni 2.1  kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.