Header Ads

RC SANARE AWATAKA VIONGOZI WA TAASISI KUZINGATIA MASLAHI YA WAFANYAKAZI.


MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, amewataka Viongozi wa Taasisi  kuhakikisha wanazingatia maslahi ya Wafanyakazi ili kuendelea kuimarisha amani.

Kauli hiyo ,ameitoa Februari 1/2021 alipokuwa akifanya ziara ya  kutembelea Shule ya Lutheran Junior Seminari iliyopo Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Sanare, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha amani inalindwa, hivyo Kama Wafanyakazi watashindwa kupata maslahi yao amani na utulivu vitaondoka.

RC Sanare, amesema katika kuona taasisi inapata mafanikio ni pamoja na Wafanyakazi kulipwa maslahi yao vizuri na kwa wakati ili kuleta matokeo chanya.

 "Tukiwanyima mishahara waalimu , tunakwenda kutengeneza bomu la upatikanaji wa matokeo mabaya Shuleni, lakini hata Shule zitakosa wanafunzi kutokana na kutokuwa na ufanisi wa ufaulu, niwaombe viongozi wa Taasisi walipe mishahara ili kuleta amani na utulivu nyumbani na Shuleni, wasipo fanya hivyo hao waalimu wakikosa utulivu wataingia barabarani  mwisho wa siku amani inaondoka, na sisi Kama viongozi wa Serikali ni kuhakikisha amani inadumishwa katika  nyanja zote, " Amesema RC Sanare.

Amewataka Waalimu wa Shule ya Sekondari Lutheran Junior Seminari, kuwa watulivu katika kipindi hiki huku akiwataka kufanya kazi kwa bidiii kwani maslahi yao watayapata na anayashughulikia kwa kushirikiana na uongozi wa Shule hiyo. 

Katika hatua nyengine, amesema lengo la ziara zake za kutembelea Shuleni ni kuhakikisha Shule zinakuwa na ufaulu, kuona mazingira ya shule , madarasa kama yanatosha kwa ajili ya watoto wanasoma. 

Amesema ataendelea na ziara hizo Shuleni ili kuona Mkoa wa Morogoro unatoka katika nafasi iliyopo ya 8 na kuwa ya juu zaidi na ikiwezekana kushuka nafasi ya kwanza Kitaifa Kama inavyofanya mikoa mingine.

"Mkoa wetu bado matokeo ya ufaulu hayaridhishi , niwaombe sana waalimu tufundishe Watoto, hii ndio kazi ambayo tumeiomba, lazima tupate matokeo makubwa, changamoto zipo lakini Serikali yetu ni sikivu Sana unaendelea kuzifuatilia na kutatua, lakini hatuwezi kupata haki Kama hatuwajibiki, haki inakuja na wajibu, tulikuwa nafasi ya 16 Kitaifa  mwaka juzi lakini tukasukumana tukafika nafasi ya 8 mwaka jana, tunataka mwaka huu tusogee angalau tuingie katika 3 Bora au ikiwezekana nafasi ya kwanza na inawezekana Kama tukitambua wajibu wetu"Ameongeza Sanare.

Amesema Sasa yupo katika kutembelea Shule zote za Msingi katika Mkoa wa Morogoro katika kuhakikisha kuwa wanafunzi walioandikishwa mwaka huu wameingia madarasani , lakini kuona waliochaguliwa Kidato Cha kwanza nao wameingia pia kwani kufikia 20 Februari wanafunzi waliofaulu wanatakiwa wawe Shuleni.

Hata hivyo , amesema baada ya kumaliza upande wa Shule za Msingi wataingia na Sekondari kufuatilia ikiwamo waliongia darasani, majengo ya  Shule pamoja na taaluma ya Shule na ufaulu katika Shule.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.