Header Ads

RC SANARE AZITAKA SHULE ZA SEKONDARI KUJIKITA KATIKA UJENZI WA MABWENI.








MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, amewataka  Waalimu wakuu kwa kushirikiana na Kamati za Shule kuanza ujenzi wa Mabweni. 

Kauli hiyo ameitoa leo Februari 21/2021 wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa Vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Kihonda.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, amesema Mabweni yatasaidia kuwaweka pamoja wanafunzi katika kujilinda na matendo hatarishi mitaani. 

RC Sanare, amesema wanafunzi wanahitaji Mazingira rafiki ya kusoma vizuri ikiwamo suala la ujenzi wa mabweni ya Shule.

 Aidha, ametaka vikao vya Kamati ya maendeleo ya Kata wawasilishe taarifa na mipango yao juu ya Ujenzi wa Mabweni ili aone  jinsi ya kuweka utaratibu mzuri wa ujenzi huo. 

Amewataka Viongozi wa Kata, Mitaa, Shule na Wazazi washirikiane vizuri ili waone jinsi ya kuanza ujenzi wa Mabweni.

"Tuanze Sasa kufikiria ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi ikiwezekana tuanze mabweni machache ya Wavulana na Wasichana, kwahiyo niwaombe Waalimu , Kamati za Shule pamoja na Wazazi shirikianeni kikamilifu ili tuone matokeo, lakini hata katika vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata ajenda ya mabweni iwe kipaumbele, ninachotaka ni kuona hiyo mikakati inaanza Sasa,Watoto hawa wakiwa na mabweni watasoma vizuri na hawatajihusisha na vitendo hatarishi ili waweze kufikia ndoto zao" Amesema RC Sanare.

Amesema kuwa, mwakani Morogoro inatakiwa kuwa na mafanikio makubwa kitaaluma na kusogea kutoka nafasi ya 8 iliyopo na kuwa ya kwanza au kuwa nafasi tatu za juu

Mwisho amepongeza juhudi za Wananchi wa Manispaa Morogoro kwa kushirikiana vizuri katika ujenzi wa Shule mpya pamoja madarasa kwani baada ya muda Manispaa Morogoro itakuwa na Shule 6 mpya za Sekondari Jambo ambalo ni mafanikio makubwa katika kuhakikisha ufaulu wa Watoto unaongezeka.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.