Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO AKANUSHA WANAFUNZI KUSOMA CHINI YA MITI

 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba (wapili kutoka kushoto) akikagua chumba cha darasa Shule ya Sekondari Bondwa , Afisa Elimu  Taaluma Sekondari Malambugi (kushoto), Afisa elimu Sekondari, Dk Janeth Barongo (wapili kutoka kulia).

Mkurugenzi wa  Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, (kulia) akiteta jambo na Afisa elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro, Dr Janeth Barongo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa .

Wanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Bondwa wakiwa darasani.

Ujenzi wa Shule mpya ya Ghorofa ya Sekondari iliyopo Kata ya Boma .

MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amekanusha kuhusu taarifa iliyosambaa ya wanafunzi wa  shule ya Sekondari Bondwa kusoma chini ya miti .

Kauli hiyo ameitoa leo, Februari 24/2021 wakati wa kukagua ujenzi wa Madarasa unaoendelea katika Shule za Sekondari kufuatia agizo la Waziri Mkuu la Wanafunzi wote wawe wamewasili shule ifikapo Februari 20/2021.

Akizungumza juu ya taarifa hiyo iliyosambaa katika mitandoa ya kijamii, Lukuba, amesema kuwa Wanafunzi waliokutwa wamekaa chini ni kutokana na waalimu wao kutaka kuwatenganisha katika mitihani ya kujipima.

“Kwa takwimu zangu nilizokuwa nazo kwa Manispaa ya Morogoro hakuna watoto wanaosomea nje, hii taarifa kiukweli nimeipokea kwa mshtuko sana nikaona nipite na wajumbe wa CMT ili kuona kama ni kweli lakini nilichokipata pale ni kwamba Mwalimu aliwapa watoto mitihani katika hali ya kuwa na uhaba wa madarasa na watoto wanapofanya mitihani waaachinae nafasi akaona awatoe nje jambo ambalo sio zuri sana lakini nilimuonya huyo mwalimu kwa mdomo na maandishi ili asirudie tena , niseme tu tupo katika hali nzuri Watoto wanasoma vizuri na wote wapo madarasani licha ya upungu wa madawati  ambao kwa sasa tunazidi kutatua changamoto ikiwamo  ujenzi wa madarasa pamoja na ujenzi wa Shule mpya 5 za Sekondari ambazo tayari zimeshaanza kujengwa ” Amesema Lukuba.

Lukuba, amesema kuwa kwa sasa changamoto kubwa ni uhaba wa madawati jambo ambalo wanaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mbunge, Madiwani ili kuhamasisha Wazazi kuchangia katika upande wa madawati.

Amesema kuwa Manispaa ya Morogoro, imeendelea kutenga fedha katika mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miundombinu ya shule za Sekondari na Msingi .

“”Mwaka wa fedha 2019/2020 tumefanikiwa kujenga madarasa 91 ya shule za msingi pamoja na madawati yake ndani, huku shule za sekondari tukijenga madarasa 16  na madawati yake, kwahiyo bado tumeendelea tena kutenga fedha katika mapato yetu ya ndani kwani mwaka huu wa fedha 2020/2021 tunatarajia kuwa na shule mpya 5 za Sekondari ambapo mpaka sasa hatua za ujenzi tayari zimeanza na zinaendelea , tumefanya hivi ni kutokana na mwitiko mkubwa wa elimu bila malipo ambapo wazazi wengi wameitikia na kuwaandikisha Watoto wao.

Aidha, amesema katiika mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia mapato ya ndani  kwa upande wa elimu ya msingi tumetenga  milioni 600, sekondari milioni 700 kuendelea na umaliziaji wa maboma, maabara na madarasa pamoja na ununuaji wa madawati.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.