DC MSULWA AHAKIKI WAFANYABIASHARA SOKO KUU KINGALU MANISPAA YA MOROGORO.
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe.Bakari Msulwa, ameongoza zoezi la uhakiki la Wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kingalu Manispaa Morogoro .
Zoezi hilo la uhakiki wa wafanyabiashara hao limefanyika Februari 13/2/2021 katika Soko hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Msulwa, amesema lengo la kuhakiki ni kutaka kutatua changamoto za wafanyabiashara ikiwamo wale waliochukua Vizimba zaidi ya kimoja, wapangishaji wa Vizimba na baadhi ya Watumishi ambao walijihusisha na kuchukua Vizimba.
Msulwa, amesema zoezi hilo linafanyika kwa siku 2 ikiwamo Jumamosi na Jumapili ambapo mara baada ya zoezi hilo taarifa zitawasilishwa kwa Mhe. Rais kufuatia maagizo yake aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa Soko hilo.
Aidha, amewataka watumishi ambao wamechukua wajisalimishe masaa 12 vinginevyo watapoteza ajira zao na kukosa Vizimba vyote kwa pamoja.
" Tumelianza zoezi hili leo Februari 13/2021, mategemeo yangu tutamaliza salama Kama wale ambao walienda kinyume na utaratibu watatupa ushirikiano, niwaombe wafanyabiashara tutoe ushirikiano na taarifa ziwe za kweli, tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza agizo la Serikali, hatuhitaji mdhaha Kama mtu atashindwa ajue tutamfikisha mahakamani ili aongee lugha nyengine zaidi ya hapa, tunachotaka haki itendeke, tunataka kizimba kimoja mtu mmoja, wale watumishi nimetoa masaa 12 umekula pesa zitapike haraka na uturudishie kizimba chetu " Amesema DC Msulwa.
Hata hivyo, amesema kuwa licha ya uhakiki huo lakini ipo Kamati iliyoandaliwa kwa ajili ya uchunguzi wa changamoto za Soko ikiongozwa na Waziri wa TAMISEMI , Mhe. Suleiman Jafo , Mkuu wa Mkoa, Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya.
Katika zoezi hilo, pia aliweza kusimamia uchaguzi wa mpito wa Viongozi Mara baada ya Uongozi wa Soko kuvunjwa na Mhe. Jafo, ambapo Uongozi huo wa mpito utaungana na Kamati kuu ili kushughulikia kero za wafanyabiashara hao.
Mwisho, amepiga marufuku wanaharakati Sokoni huku akisema hao ndio wanaochelewesha maendeleo.
"Sitaki kuona wanaharakati humu ndani, hawa ndio wanatuchelewesha kukichwa mabarua wanahangaika na mabarua na kuwashawishi wenzao kuwa na migomo isiyo na tija, ninachotaka ni kuona tunapata Uongozi mzuri shirikishi ambao utasimama imara kuhakikisha Soko letu linakwenda mbele na malengo ya Serikali yanatimia, Uongozi ni mmoja tu tutakao utaka hawa wanaojiita wanaharakati wakatafute Soko lao siwataki humu ndani, nikiwakuta tutaimba nao wimbo mwengine mbele tumechelewa Sana tunahitaji kupiga hatua sio kila siku migogoro ambayo wapo Watu wachache tu wanao tuharibia"Ameongeza DC Msulwa.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wafanyabiashara kuwa wakweli ili kufanya zoezi hilo kuwa jepesi.
" Niwaombe wafanyabiashara tuwe wakweli na taarifa zetu, hili ni zoezi nyeti Sana na maagizo ya Serikali ukishindwa kutupa ukweli , ipo Mahala ambapo utaenda kusema ukweli, tunachokitaka sisi kero ziondoke tufanye kazi, Soko hili ni lenu, hatuwezi kufikia malengo Kama huku mna minung'uniko , tunataka Soko liwe tulivu na malengo ya Serikali yatimie" Amesema Mhe. Kihanga.
Kwa upande wa Mkurugenzi Manispaa Morogoro,Sheilla Lukuba, amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kusimamia zoezi hilo huku akimuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha na kupokea maelekezo yatakayotolewa.
Lukuba , amesema Soko limejengwa kwa fedha za Kodi za Wananchi, hivyo ni vizuri hao Wananchi wakaendelea kunufaika na mradi huo bila ya changamoto.
" Zoezi ni zuri , nampongeza Mkuu wa Wilaya, na Kamati ya ulinzi na usalama, nipo tayari kupokea maelekezo ili mradi utulivu uendelee , na wale ambao bado wanaweka msimamo mkali sisi maelekezo yakija hatutawafumbia macho" Amesema Lukuba.
Zoezi hilo lililofanywa leo limehusisha wafanyabiashara ambapo ni waasisi waliopisha Ujenzi wa Soko Jipya wapatao 470, lakini Februari 14/2021 zoezi hilo la uhakiki wa Vizimba na Vioski litaendelea tena katika Soko hilo.
Post a Comment