RC SANARE AAGIZA HALMASHAURI KUJIKITA KUPAMBANA NA AFYA DUNI ZA WATOTO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare (kulia) akiongoza Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe mfuko wa afya ya Jamii (iCHF).( kushoto) Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Eng. Emanuel Kalobelo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Eng. Emanuel Kalobelo akifuatilia kwa makini Mkutano wa tathmini ya Mkataba wa lishe .Afisa Lishe Mkao wa Morogoro Salome Magembe akitoa taarifa za hali ya Lishe.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, ameziagiza halmashauri zote za wilaya mkoa wa Morogoro na wadau wa afya kuongeza jitihada,mikakati na raslimali katika kujikita kupambana na afya duni za Watoto.
Sanare, ametoa agizo hilo leo Jumatano Februari 03/2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mezanine Jengo la NSSF Manispaa ya Morogoro akifungua Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe Mfuko wa afya ya Jamii (iCHF).
Aidha, amesema kuwa , takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Morogoro unashika nafasi ya 3 katika hali ya Lishe , hivyo amezipongeza Halmashauri ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mktaba wa Lishe katika kupambana na afya duni za Watoto.
“Niwapongeze sana Manispaa ya Morogoro kwa kuwa washindi wa utekelezaji wa mkataba wa lishe, lakini na zile Halmashauri zilizofanya vizuri pia kwa kushirikiana na wadau wa lishe, lakini nawapongeza sana watoa huduma ngazi ya jamii na ngazi ya Vituo vya kutolea huduma, kwakweli kwa haya niliyoyaona mmefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha Mkoa wa Morogoro unatokomeza watoto wenye udumavu, ombi langu endeleeni kupambana ikiwemo kutoa elimu mara kwa mara ili huduma hii iweze kutekelezeka vizuri katika Jamii”Amesema RC Snare.
Hata hivyo, amesema kuwa bado Mkoa wa Morogoro unakabiliwa na tatizo la lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano na akina mama walio kwenye umri wa kuzaa na kusisitiza kuwa kila mmoja anatakiwa kuwajibika kukabiliana na changamoto hiyo.
Amesema kuwa , Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikichukua hatua za kukabiliana na utapiamlo Mkoa wa Morogoro ikiwemo kusaini mkataba wa utendaji wa masuala ya lishe kati ya mkuu wa mkoa,wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri,watendaji wa kata na vijiji ili kufuatilia viashiria vya lishe.
“Natoa wito kwa wadau wote wa afya ndani ya mkoa wetu kuendelea kushirikiana na serikali kutekeleza mipango mbalimbali iliyopo ili kuinua viashiria vyote vya lishe. Narudia tena kuziagiza halmashauri zote katika kipindi hiki cha maandalizi ya Mipango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zitenge shilingi 1,000 kwa kila mtoto aliye chini ya miaka mitano kwenye mapato ya ndani”,Ameongeza RC Sanare.
Hata hivyo, ameziagiza Halmashauri kuweka mikakati ya kuongeza kiwango cha uandikishaji wa kaya katika Mfuko wa Afya ya Jamii ‘CHF iliyoboreshwa’ ili wananchi wafurahie huduma za kiafya kupitia CHF.
“Nawashukuru wadau wote kwa michango na misaada yenu mnayotoa katika kuboresha huduma za afya na lishe. Naomba muendelee kushirikiana na mkoa wetu ili tuweze kukabiliana na changamoto zinazotukabili katika utekelezaji wa afua za afya. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na lishe” Ameongeza RC Sanare.
Mara baada ya uwasilishwaji wa tarifa za lishe, Afisa Lishe Mkoa wa Morogoro, Salome Magembe, alizitaja halmashauri zilizopata vyeti vya ushindi kutokana na kutekeleza vyema mkataba wa lsihe katika Halmashuri , ambapo Manispaa ya Morogoro iliibuka kinara mshindi wa kwanza kwa wastani wa asilimia 90.5, Mvomero asilimia 90.4 na Kilosa asilimia 86.1.
“Halmashauri zilizopata vyeti vya ushindi kutokana na kutekeleza vizuri mkataba wa lishe na kutambua mchango wao katika kuinua kiwango cha kaya kujiunga na CHF iliyoboreshwa ni Manispaa ya Morogoro, Halmashauri ya Mvomero, na Kilosa, ni waase Maafisa Lishe wa Halmashauri pamoja na watoa huduma ngazi za Kata tushirikiane kwa pamoja katika kutokomeza na kupambana na afya duni za Watoto" Amesema Magembe.
Magembe, amesema kuwa vyeti ambavyo vimetolewa kwa washindi ni kutokana na Bajweti ya mwaka wa fedha ya 2019/2020 katika kutekeleza viashiria vya Mkataba wa Lishe.
Post a Comment