Header Ads

BARAZA LA WAFANYAKAZI SEKRETARIETI YA MKOA WA MOROGORO LAPITISHA BAJETI 2023/2024.


Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro wamepitisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo takribani 11,873,795,000 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.

Bajeti hiyo imepitishwa Machi 9 mwaka huu na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro kwenye ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Akisoma mpango wa bajeti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro mbele ya wajumbe wa kikao hicho Afisa Bajeti kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Bw. Erick Ulomi amesema kati ya fedha hizo shilingi 8,079,813,000 zitaelekezwa kwenye matumizi ya kawaida ambayo yanajumuisha shilingi 3,776,918,809 kwa ajili ya mishahara na shilingi 4,243,316,000 ni matumizi mengineyo.

Aidha, Katika kikao hicho wajumbe wamependekeza suala la ajira  kwa wafanyakazi wapya kwa kada mbalimbali lipewe kipaumbele ili kuziba mapengo  ya watumishi yaliyotokana na kustaafu, kifo na kuhama kwani kasi ya kupungua watumishi kwa kila kada ni kubwa kuliko kasi ya kuajiri na hivyo kuathiri utendaji kazi katika ofisi mbalimbali.

Sambamba na hilo, wajumbe hao pia wameshauri Mkoa kujenga hoja na kuwasilisha hoja hizo ngazi ya Taifa ili kuongezewa Bajeti ya Mkoa kutokana na ukubwa wa Mkoa ukilinganisha na baadhi ya mikoa mingine pamoja na changamoto nyingine zinazojitokeza ndani  ya Mkoa huo.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya  UTAWALA  aliwataka wajumbe wa kikao hicho kupitia kwa makini wasilisho la bajeti hiyo na kutoa maoni yao ili kuboresha bajeti hiyo kabla ya kuwasilishwa na kuidhinishwa na bunge lÃ¥ Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Sekretarieti ya Mkoa huo iliidhinishiwa kutumia shilingi 11,873,795,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mmaendeleo, Kati ya fedha hizo shilingi 8,079,813,000 zilitengwa kwa ajili matumizi ya kawaida zilizojumuisha shilingi 3,836,497,000 kwa ajili ya mishahara na shilingi 4,243,316,000 matumizi mengineyo.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.