MBUNGE MZERU AAHIDI MILIONI 1.5 KUTUNISHA MFUKO WA JUKWAA LA WANAWAKE KIHONDA KUJIKWAMUA KIUCHUMI
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Norah Mzeru, ameahidi kuwapatia Jukwaa la Wanawake Kata ya Kihonda Shilingi milioni 1 na laki 5 kwa ajili ya kutunisha mfuko wa jukwaa lao katika kujikwamua kiuchumi.
Ahadi hiyo ameitoa Machi 04/2023 akiwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kata ya Kihonda.
Akizungumza na Wanawake hao, Mzeru, amesema lengo ni kuona wanawake wanafanikiwa na kusonga mbele.
Kuhusu mradi wa uchakataji wa Chupa za plastiki, Mhe. Mzeru, ameahidi kuwapa shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kuongezea katika ununuzi wa mashine ya uchakataji huku akisema shilingi laki 5 zitaingia kama mchango wa kutunisha mfuko wa Jukwaa kwani anafahamu malengo waliyokuwa nayo wakina mama hao.
"Nimeguswa na miradi yao hususani huu wa uchakataji chupa za plastiki, nimeahidi kuwapa milioni 1 waongeze katika ununuzi wa mashine hiyo, lengo ni kuona wakina mama Kihonda wanakuwa ni wa mfano Kimkoa kuweza kuwa na kiwanda kitakachowasaidia kujiari na kupata mapato” Amesema Mzeru.
Mzeru ,amesema Kiwanda hiko cha uchakataji kitachangia kutoa mchango mkubwa wa kuinua uchumi wa akina mama wa Kihonda na kutoa ajira kwa wengine.
Aidha, amesema mradi huo wa uchakataji chupa za plastiki ni hatua ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na pia kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhimiza kuhusu Sera ya Viwanda na akiwa kama Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro ni wajibu wake kuwa karibu na wananchi kuwasaidia kwa kutoa mchango wake .
Hata hivyo, amewataka Wazazi kuwa karibu na Watoto wao ili kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Diwani wa Kata ya Kihonda, Mhe. Hamisi Kilongo, amelipongeza Jukwaa kwa kuandaa shughuli kubwa pamoja na kumpongeza Mhe. Mzeru kwa msaada wake kwa wanawake hao.
Diwani wa Viti Maalum na Katibu wa Madiwani Manispaa ya Morogoro, Mhe. Salma Mbando, amesema Mhe. Mzeru amekuwa mtu wa kujitoa hivyo wakina mama wanakila sababu ya kumpongeza na kutimiza ndoto zao bila kumwangusha kwa masaada alioahidi kutoa.
Kwa upande wa Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kihonda, Germina Matotay , amesema Kata hiyo imenufaika na mkopo wa asilimia 10 wa Manispaa ya Morogoro ambapo jumla ya Milioni 88,260,00 zilitolewa katika vikundi 16 kutoka mwaka 2015-2023 na kwa sasa vikundi vyote vinajishughulisha na miradi ya Viwanda vidogovidogo, biashara ndogondogo na kuweka na kukopeshana.
Matotay, amesema Jukwaa linatarajia kuwa na miradi ya uchakataji wa chupa za plastiki, pamoja na utengenezaji wa batiki pamoja na usindikaji mafuta ya alizeti ambapo miradi hiyo itaanza mara baada ya kupata mkopo ambao wanatarajia mwaka 2023 kuanza shughuli zake.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kihonda , Mwamin Daud , amemshukuru Mhe. Mzeru, kwa ahadi yake ya kuchangia ununuzi wa mashine kwa kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha uchakataji ambacho kitasaidia kuwakutanisha wanawake na vijana wakike kujifunza ujuzi wa uchakataji wa chupa ambao utawasaidia katika maisha yao ya kijamii na kiuchumi.
Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2023 " MABADILIKO YA TEKNOLOJIA , CHACHU KATIKA KULETA USAWA WA KIJINSIA".
Post a Comment