DIWANI LUJUO MBIONI KUMALIZIA UKARABATI UJENZI KITUO CHA POLISI KATA YA BOMA
DIWANI wa Kata ya Boma Manispaa ya Morogoro, Mhe. Athumani Lujuo, amesema anatarajia kumalizia ukarabati wa Kituo cha Polisi Kata ya Boma kwa lengo la kuimarisha ulinzi katika Kata hiyo.
Kauli hiyo, ameitoa leo Machi 03/2023 kupitia njia ya simu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo Kata ya Boma imeadhimisha leo kwa kufanya usafi katika eneo la Ofisi ya Kata, eneo la shule mpya ya Sekondari ya Ghorofa pamoja na eneo la Ofisi ya Kituo cha Polisi Kata.
Mhe. Lujuo, amesema lengo la ukarabati huo ni kuhakikisha kuwa Kata hiyo inakuwa na Kituo cha Polisi ngazi ya Kata kwa ajili ya kuimarisha hali ya ulinzi kwa wananchi wa Kata yake.
" Kituo hiki hakijatumika zaidi ya miaka 5 sasa, hata jengo lake lilikuwa chakavu sana na ni finyu, ukarabati ambao ninaendelea kuufanya ni pamoja na kupanua miundombinu ya vyumba vya Ofisi , ulinzi ni jambo la Msingi, Polisi Kata wetu hana makazi maalumu ya kufanya shughuli zake, nimeona nifanye ukarabati huu kisha nimkabidhi Ofisi yake kwa ajili ya kuendelea na utekekelezaji wa majukumu yake" Amesema Lujuo.
Ukarabati unaofanyika kwa sasa ni upanuzi wa Jengo kwa kuongeza vyumba vya Ofisi, upauaji, uezekaji pamoja na uingizaji wa vitu vya samani.
Aidha, amesema mara baada ya Kituo hicho kukamilika na kufanya kazi, atakabidhi Pikipiki 1 kituo hicho kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi.
Naye, Polisi Kata ya Boma, Inspekta.Pendo Meshurie, amempongeza Diwani huyo kwa kuwajengea Ofisi.
"Tunampongeza sana Mhe. Diwani kwa kutujali , bado makazi yetu sio rasmi tunafanya kazi katika Ofisi ya Kata hivyo tunaamini ujenzi huo utatusaidia sisi kufanya kazi zetu vizuri kwa ufanisi, tunamshukuru , kikubwa tunamuahidi kuendelea kusimamia hali ya ulinzi na usalama, Kata yetu ipo shwari , kikubwa wananchi pia waendelee kutupa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yetu, jukumu la ulinzi sio la Polisi tu bali ni wananchi wote" Amesema Inspekta Meshurie.
Post a Comment