MAAFISA UGANI MKOA WA MOROGORO WAKABIDHIWA PIKIPIKI 436
MAAFISA Ugani Mkoa wa Morogoro wamekabidhiwa Pikipiki 436 kutoka Wizara ya Kilimo ambapo Mkoa wa Morogoro ukiwa ni miongoni mwa mikoa 15 inayopokea pikipiki kwa awamu ya pili.
Tukio hilo la kukabidhi Pikipiki , lemefanyika Machi 27/2023 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Nsemwa amekabidhi Pikipiki hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Nsemwa, amesema lengo la Serikali kutoa Pikipiki hizo kwa Maafisa Ugani ni kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakuwa na tija pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.
" Leo tumegawa Pikipiki hizi, tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kugawa pikipiki hizi, nitoe wito kwa Maafisa Ugani wote kuhakikisha wanazitumia kwa shughuli za ugani ili kuhakikisha kuwa Kilimo katika Mkoa wetu kinaboreka zaidi na kuchangia katika uchumi wa mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla|"Amesema DC Nsemwa.
DC Nsemwa, amesema Mkoa wa Morogoro umepokea jumla ya pikipiki 436 kati ya hizo Pikipiki 306 zimepelekwa moja kwa moja katika Halmashauri husika ambazo ni Mvomero pikipiki 99, Kilosa 87, Morogoro DC 68 na Halmashauri ya Mji Ifikara 52.
Aidha,amesema jumala ya Pikipiki 130 zimekabidhiwa Mkoani kwa ajili ya Halmashauri za Mlimba pikipiki 34, Ulanga 27, Gairo 26, Malinyi 20, Manispaa ya Morogoro 20 na Mkoani pikipiki 3.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amempongeza Mhe. Rais ,Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kugawa vitendea kazi zikiwemo Pikipiki, vifaa vya kupimia afya ya udongo, vishikwambi na visanduku vya ugani kwa Maafisa Ugani Kilimo nchini kwa lengo la kuimarisha na kuboresha huduma za ugani nchini.
Machela amewataka Maafisa Ugani Manispaa ya Morogoro kuzitunza na kuzihudumia pikipiki hizo ili zidumu na kuleta tija.
Kwa upande wa Afisa Ugani Manispaa ya Morogoro , Wanted Mmari, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutatua changamoto ya Maafisa ugani katika utoaji wa huduma kwa wakulima huku akisema kuwa kwa sasa wakulima watapata huduma kwa wakati Kwa kuwa uwezo wa kuwafikia umeimarishwa.
Post a Comment