Header Ads

JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA MOROGORO MJINI YAFANYA ZIARA SHULENI, YARIDHISHWA NA UETEKELEZAJI WA ILANI YA CCM KATIKA SEKTA YA ELIMU.


 


JUMUIYA ya Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, imeridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)   kwa upande wa Idara ya Elimu Msingi  katika Manispaa ya Morogoro.

Hayo, yameyabainisha hivi karibuni Machi 1/2023  katika ziara ya Kamati ya Utekelezaji Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini  iliyoambatana  na Kamati ya Elimu na Malezi Wazazi Wilaya.

Akiongea katika ziara hiyo,Mwenyekiti wa Wazazi CCM Wilaya, CDE. Salum  Kipira, amesema lengo la ziara shuleni  ni kuhakikisha wanapata  maelezo sahihi na ya kina kama sehemu ya kujifunza ili wakatoe  elimu kwa wanachama wao  wa Jumuiya ya Wazazi inayosimamia Elimu, Malezi, Mazingira, Afya pamoja na Utamaduni.”

Aidha , Kipira, amesema  kamati ya utekelezaji imeridhishwa  na mwenendo wa Elimu katika Manispaa ya Morogoro licha ya kuwepo kwa changamoto shuleni ambazo anaamini kama viongozi waliopewa dhamana ya kiutendaji wakitupia macho huko wanaamini matatizo hayo yatatatuliwa .

"Ziara yetu ilikuwa ya kupita shuleni, kuona namna Ilani inavyotekelezwa , ombi letu sisi Wazazi ambao tunafanya kazi moja kwa moja na Taasisi za Elimu, kubwa tunaomba utoro mashuleni ushughulikiwe pamoja na mwenendo wa maadili kwa wanafunzi wa rika huku tukiwataka wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupewa kipaumbele ili waweze kusoma katika mazingira rafiki kama wanafunzi wengine, na hizi changamoto nyengine kama vile vyoo na uchakavu wa madarasa viongozi wapo waliangalie kwa jicho la tatu lengo watoto wetu wasome mazingira rafiki na kutimiza ndoto zao kama Ilani ya CCM inavyotaka " 

Katika hatua nyengine, Kipira, amempongeza  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ,kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuboresha sekta ya Elimu Nchini kwani amekua akifanya jitihada za juu sana kuhakikisha anatoa fedha kwaajili ya ujenzi wa madarasa lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu kwenda Sekondari waweze kusoma katika miundombinu rafiki ili kukuza sekta ya elimu nchini.

Upande wa Katibu Elimu Malezi Wazazi CCM Wilaya, Ndg. Godwin Mlambiti, ameahidi kuendelea na ziara kadri Kamati ya utekelezaji itakavyomuagiza ili kusikiliza changamoto za elimu ikiwemo maadili ya watoto kuanzia shuleni na maeneo ya Jamii. 

Naye mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi Wilaya, Kibibi Makumbo, katika kuguswa na changamoto za madarasa, ameahidi kutoa mifuko 30 ya saruji katika shule ya Msingi Sultan Area.

Licha ya hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu na Malezi, Blantina Chibinda, amesema kwa kushirikiana na Katibu Elimu Malezi wa Wilaya wao kama kamati wataendelea kutoa ushirikiano mkubwa kuona suala la malezi shuleni lina imarika lakini wanafunzi wanakuwa na maadili pamoja na kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia ambapo vimeonekana kushamiri kila uchwao.

Ziara ya Kamati ya Utekelezaji ilianza Machi 01/2023 , miongoni mwa shule zilizotembelewa ni Shule za Msingi Mafiga A na B, Shule ya Msingi Sultan Area, Shule ya Msingi Kihonda Maghorofani , Shule za Msingi Mazimbu A na B pamoja na Shule ya Msingi Sabasaba iliyopo Kata ya Kiwanja Cha Ndege.

Ziara ya kuzunguka katika shule bado inaendelea ambapo Machi 06/2023 itakuwa katika Kata ya Mkundi na Kata nyengine taarifa zaidi zitatolewa.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.