Header Ads

DC NSEMWA AWATAKA WANANCHI KUFICHUA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA.



MKUU wa wilaya ya  Morogoro, Mhe.  Rebecca Nsemwa , amewataka wananchi kuisaidia serikali katika kutoa taarifa za kweli zitokanazo na ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa na kulawitiwa.

Kauli hiyo ameitoa   Machi, 22/ 2023 katika ziara ya kamati ya siasa CCM wilaya ya Morogoro yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali katika kata mbalimbali.

DC Nsemwa, amesema kuwa kesi nyingi za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia zimekua na mwisho usioridhisha kutokana na baadhi ya walalamikaji kumaliza wenyewe mgogoro baina yao nyumbani na kuficha ushahidi ambao ungesaidia kumuweka mtuhumiwa hatiani

“Inauma sana pale ambapo mtoto  amefanyiwa ukatili halafu wazazi  au walezi wa mtoto huyo kukubali kupokea rushwa ndogo kutoka kwa mtuhumiwa na kusahau madhara yanayoweza kuendelea kutokea kwa mtoto na jamii kwa ujumla  kwa hiyo tubadilike, tunapoona matendo kama haya tuyakemee na kuyafichua tusiyakalie kimya ”Amesema DC Nsemwa

Aidha , amesema Ofisi yake ipo wazi hivyo wanapoona vitendo vya ukatili wawasiliane nae moja kwa moja kupitia namba yake ya simu ili aweze  kulifatilia kwa karibu tukio hilo  na kuhakikisha haki inapatikana na kukomesha ukatikili huo katika jamii.

Pamoja na hayo Nsemwa amewaomba Viongozi wa chama kushirikiana na kamati za shule kuhamasisha wazazi kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana shuleni, hali ambayo ni muhimu katika kustawisha utulivu darasani ambao unaweza kua chanzo cha kukatiliwa kijinsia kama hautazingatiwa .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma, amewataka watendaji wa kata kwa kushirikiana na viongozi wa Chama kuwa kipaumbele kwa kuhamasisha jamii juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao kama vile maji,umeme,afya na elimu.

Mwisho, Fikiri, ameendelea kutoa shukrani za dhati kwa Viongozi wote wa Chama na Serikali katika kuendelea kutekeleza na  kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM  ili kufikia malengo yaliyo kusudiwa.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.