Header Ads

DIWANI BIDYANGUZE AELEZA MAFANIKIO KATA YA KINGOLWIRA KWA KAMATI YA SIASA YA KATA HIYO.


DIWANI wa Kata ya Kingolwira Manispaa ya Morogoro ,Mhe. Madaraka Bidyanguze, ameeleza mafaniko ya Kata ya Kingolwira katika sekta ya Elimu , afya na miundombinu.

Mh. Bdyanguze, ameyasema hayo wakati wa kuwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika  ziara ya Kamati ya Siasa ya Kata hiyo ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo  Machi 23/2023.

Akizungumza wakati akisoma taarifa za maendeleo ya miradi , Mhe. Bidyanguze, amesema Kata ya Kingolwira, katika sekta Elimu   imefanikiwa kwa kiasi kikubwa hususani katika ujenzi wa madarasa upande wa elimu Sekondari kupitia fedha za Pochi la Mama ambapo Uongozi wa Kata umeweza kusimamia kikamilifu ujenzi wa madarasa hayo.

Amesema katika upande wa madarasa ya pochi la Mama , Shule ya Sekondari Kingolwira iliingiziwa Milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 3 ambayo yamekamilika na wanafunzi wameshaanza kuyatumia.

Aidha, amesema licha ya fedha za pochi la mama, lakini Shule ya Sekondari Kingolwira iliingiziwa milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 4 kupitia fedha za Uviko 19 ambayo nayo yanatumika.

"Haya ni maendeleo ambayo tuna haki ya kuyasema, Mhe. Rais ameweka fedha nyingi katika Kata yetu lazima tumpongeze, lakini Manispaa kupitia fedha za ndani wametuletea fedha ambazo asilimia kubwa zimetumika katika ujenzi wa madarasa mapya katika Shule ya Msingi Kingolwira" Amesema Mhe. Bidyanguze.

Pia, amesema upande wa Shule ya Sekondari Kingolwira, tayari mpaka sasa shule hiyo imeweza kujenga vyumba 2 vya Maabara yaani Maabara ya Physics , Biology  na Chemistry.

Upande wa huduma za afya, amesema Mradi wa Maabara kubwa ya kisasa ambayo kwa sasa imefikia asilimia 95 ambapo mara baada ya kukamilika kwake itakuwa Maabara kubwa kuliko zote Manispaa na itaweza kuhudmia wateja wengi zaidi na kuongeza mapato katika Kituo cha Afya cha Kata hiyo.

" Maabara yetu inakwenda kutoa huduma kubwa ndani ya mwezi mmoja ujao, tunaamini kabisa tutwahudumia watu wengi, ndiyo maabara kubwa na ya kisasa kwa Manispaa yetu ya Morogoro, hata kichomea taka chake ni cha kisasa ambacho nacho kitaweza kutoa huduma ya uchomaji taka zote kwa ukubwa zaidi na tutahudumia Vituo vya afya na Zahanati zote ambazo zitahitaji huduma kwetu ya uchomaji wa Taka na huu pia ni mpango ambao utaongeza mapato katika Zhanati yetu ya Kingolwira" Ameongeza Mhe. Bidyanguze.

Hata hivyo, kuhusu vivuko, amesema kutokana na changamoto waliyokuwa wakiipata wananchi , walitengeneza vivuko 2 ambavyo leo vimekuwa vikitumika kwa ajili ya usafiri na barabara hiyo yenye vivuko ipo mbioni kuunganishwa ili iwe barabara ya kiunganishi  kwa watu wanaoishi Kata ya Mkundi.

Kuhusu Ujenzi wa Ofisi ya Kata, amesema wamehamia  Ofisi mpya lakini bado Ofisi hiyo inahitaji maboresho ili ikamilike kwa asilimia 100.

Amesema kuwa  serikali kupitia Ofisi yake ya Kata kwa kushirikiana na Wataalamu pamoja na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM watahakikisha wanaendelea  kusimamia miradi yote ya maendeleo ili fedha zinazotolewa na serikali zipate thamani yake kwenye miradi hiyo na kuweza kusogeza huduma bora zaidi kwa wananchi.

Akielezea Idara ya Maendeleo ya Jamii ,amesema Vipo vikundi ambavyo vimeshakopeshwa kupitia fedha za mkopo wa asilimia 10 zinazotolewa  na Manispaa, hivyo amewataka wananchi wake wafuate taratibu kwa kuunda vikundi na kusajili mili waweze kupata mkopo.

Akizungumzia Ulinzi na Usalama, amesema kwa sasa Kata hiyo ipo salama huku akiwataka wananchi kuendelea kufanya kazi kwa amani  bila ya uwoga kwani usalama upo wa kutosha.

Miongoni mwa miradi ya Maendeleo ambayo ameionesha kwa Kamati ya Siasa ya Kata ni pamoja na Jengo la Ofisi ya Kata, Kivuko cha Kitungwa, Madarasa shule ya Msingi Kingolwira, Ujenzi wa Jengo la Maabara ya Kisasa Kituo cha afya cha Kingolwira na kichomea taka cha kisasa pamoja na ujenzi wa madarasa ya Pochi la mama na madarasa ya Uviko pamoja na Maabara zilizopo Shule ya Sekondari Kingolwira.









No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.