HALMASHAURI YA WILAYA YA BAGAMOYO YAPONGEZA MANISPAA YA MOROGORO KWA HATUA KUBWA YA UKUSANYAJI MAPATO NA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bagamoyo, imeipongeza Manispaa ya Morogoro kwa ukusanyaji wa mapato pamoja na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo ajili ya Wananchi wa Manispaa hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 21/2023 wakati wa ziara ya Viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Mohammed Usinga aliyeambatana na Waheshimiwa Madiwani pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo ,Mhe. Usinga, amesema kuwa kitendo cha Manispaa ya Morogoro kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na ukusanyaji mkubwa wa mapato ya ndani ni moja ya hatua kubwa ya kuhakikisha ya kwamba wananchi wanapata huduma bora.
Mhe. Usinga, amesema kuwa wamejifunza mambo mengi mazuri ambayo hapo awali walikuwa hawayafahamu hivyo kwa namna moja au nyingine yatabadilisha utendaji wao wa kazi na kuleta matokeo chanya katika Halmashauri yao.
“Tumejifunza mambo mengi ambayo tulikuwa hatuyafahamu hapo awali. Tumejifunza namna bora ya ukusanyaji wa mapato, usimamiaji wa masoko, usimamiaji wa sheria ndogo ndogo za ukusanyaji wa mapato, namna bora ya kuwapanga wafanyabiashara ndogo ndogo katika masoko ili iwe rahisi kukusanya ushuru na namna bora ya utunzaji wa mazingira. Nina imani haya yote tuliyojifunza tukiyaweka kwenye utekelezaji tutakuwa tumepiga hatua kubwa" Amesema Mhe. Usinga.
Aidha, Mhe. Usinga, ameushukuru Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa mapokezi makubwa, na akapongeza juhudi za Manispaa hiyo katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo pia kuimarisha ukusanyaji wa mapato yake ya ndani.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pscal Kihanga, amesema kwa mwaka Manispaa ya Morogoro inakusanya zadi ya Bilioni 12 hivyo kuongezeka kwa vitega uchumi vitasaidia kuongeza Zaidi pato la ndani la Manispaa.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Gabriel Paul, amesema mafanikio ya Manispaa ya Morogoro yametokana na ushirikiano baina ya Madiwani kwa kushirikiana na Watumishi ambapo kutokana na ushirikiano huo ndio chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa mapato ya ndani.
Katika ziara hiyo ya siku mbili ,Wujumbe hao waliweza kutembelea Soko Kuu la Chifu Kingalu pamoja na Stendi ya Mabasi Msamvu.
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imekuwa ikipokea wageni mara kwa mara wanaokuja kujifunza namna inavyotekeleza majukumu yake na kupata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali kama ukusanyaji mapato.
Post a Comment