KATA YA SABASABA YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE KWA KUWAKUMBUKA WATOTO WENYE UHITAJI
KATIKA kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani, Kata ya Sabasaba Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Vikundi vya wanawake wameadhimisha siku hiyo kwa kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalum shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
Maadhimisho hayo yamefanyika Machi 8/2023 yakiambatana na Maandamano.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Diwani wa Kata ya Sabasaba ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Mohamed Lukwele, amesema wadau wamependekeza shule hiyo kwa kuwa ina watoto ambao hawana uwezo wa kusikia na baadhi ambao hawana uwezo wa kuona vizuri.
“Shule hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa mahitaji kama vile pempapasi ambapo wengine wamekuwa wakitokwa na haja , zipo changamoto nyingi nyingi sana kwa kutambua hilo ndugu zetu wanavikundi wameona watutembelee tunawashukuru sana kwani walichokitoa sisi kwetu ni kikubwa" Amesema Lukwele.
Upande wa Kaimu Mtendaji Kata ya Sabasaba , Abubakari Dikungule, ameshukuru wadau hao na kuomba kuendelea kujitoa kwa watoto wenye uhitaji.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Sabasaba, Asnaty Dibwe, amevishukuru vikundi vya Msimamo B Vikoba na Sabasaba Women kwa mahitaji ambayo wametoa kwa watoto hao na kuwafanya watoto kufarijika na kuwatoa katika upweke na wao kutambua wapo wanaowajali.
Mwakilishi wa Vikundi hivyo, Bi. Velda Msangi, amesema wameguswa na uhitaji wa watoto katika shule hiyo, hivyo watajipanga kuona namna ya kutoa zaidi ya hapo.
Aidha, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Dotto Kangeta , amevishukuru vikundi pamoja na Mhe. Diwani na Uongozi wa Kata kwa kuifanya shughuli hiyo katika shule yake na kutoa wito kwa wadau wengine kuwakumbuka watoto wenye uhitaji ili waweze kufarijika na mwisho kutimiza malengo yao.
Post a Comment