Katibu Mkuu wa CCM atoa maagizo haya kwa Shirika la Umeme Tanzania ‘TANESCO’
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo ,ametoa mwezi mmoja kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),mkoani Singida kufikisha umeme kwa mwekezaji kampuni ya Alfardaws inayotekeleza mradi wa kilimo cha alizeti katika Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.
Agizo hilo amelitoa leo ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Singida, akiambatana na sekretarieti ya CCM baada ya mwekezaji, Anass Kaseeh wa kampuni hiyo kutoka Jordan kuomba kufikishiwa umeme, kwani tangu wafanye maombi bado hawajafanikiwa.
“Kampuni yetu ya uwekezaji tumesajiliwa hapa nchini mwaka 2021 kwa mujibu wa sheria na taratibu zote, tumeshaomba kuletewa umeme, lakini bado hatujafanikiwa kuupata”-
“Tumeshachimba visima vitatu vya maji kati ya 24 vinavyohitajika na mfumo wetu wa umwagiliaji katika mradi unahitaji umeme mkubwa, ila hadi sasa bado umeme haujafika, tunaomba serikali itusaidie na sisi uko tayari kutoa ushirikiano kurahisisha ufike,”amesema Kaseeh.
Chongolo akizungumzia tatizo hilo amesema uwekezaji huo ukitekelezwa unafungua fursa nyingi mkoani humo na kutoa ajira kwa wananchi na kusema ni lazima huduma ya umeme ifike kwa haraka na kuagiza ndani ya mwezi mmoja wahusika waufikishe.
Post a Comment