DIWANI MATESA AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI JUMUIYA YA WAZAZI, AAHIDI KADI 100 NA BIMA ZA AFYA BURE KWA WAJUMBE WA BARAZA KATA WAZAZI ,NA VITENDEA KAZI KWA MAKATIBU WA JUMUIYA.
DIWANI wa Kata ya Uwanja wa Taifa, Mhe. Rashid Matesa, ameipongeza Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuimarisha uhai wa chama.
Kauli hiyo ameitoa Februari 24/2023 katika Mkutano wa Baraza la Wazazi CCM la Kata ya Uwanja wa Taifa.
Matesa, amesema kuwa kwa sasa Jumuiya imeonekana kuwa moto sana jambo ambalo linampa faraja kubwa ya kuona sasa Chama kinaendelea kuimarika kupitia Jumuiya hiyo.
Aidha, Mhe. Matesa, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma za afya nchini.
Amesema katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro zaidi ya Bilioni 3.3 , Rais Samia amezielekeza katika ujezi wa madarasa, na zaidi ya Bilioni 1.5 zimeshatolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya , mambo ambayo ni makubwa katika historia ya Tanzania.
" Sisi Manispaa ya Morogoro tumeletewa zaidi ya Bilioni 3.3 katika Ujenzi wa madarasa zaidi ya 150, katika fedha hizo awali tuliletewa Bilioni 1.7 fedha za UVIKO na Bilioni 1.6 ni fedha za Pochi la Mama, Bilioni 1.5 tumepokea ujenzi wa Hopsitali ya Wilaya, huu ni upendo ambao Rais ametuoneshea sisi wana Manispaa ya Morogoro" Amesema Matesa.
Hata hivyo, Matesa, amesema katika Kata yake ya Uwanja wa Taifa kwa sasa huduma ya Zahanati ipo mbioni kwani wanakamilisha ujenzi wa Zahanati mpya ambayo inatarajia kukamilika katika mwaka huu wa fedha 2022/2023.
Katika kuimarisha uhai wa Chama, ameahidi kugawa kadi 100 kwa Wanachama wa Jumuiya ya Wazazi pamoja na kuwapatia Bima za afya kwa Wajumbe wa Baraza la Wazazi Kata Uwanja wa Taifa pamoja na kugawa vitendea kazi kwa Makatibu wote wa Jumuiya ya Wazazi.
" Kwenye upande wa Bima nitaliweka sawa, hapa wanaostahili ni wale Wajumbe wote wa Baraza la Wazazi Kata, ili waweze kutibiwa na kupata huduma bora, lakini upande wa kadi naanza na kadi 100 lakini tutaendelea kufanya hivi kadri tunavyojaliwa," Ameongeza Matesa.
Aidha, amesema mara baada ya Zahanati ya Uwanja wa Taifa kukamilika itakuwa imewasogezea wananchi huduma karibu.
Naye, Katibu Elimu na Malezi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Ndg. Godwin Mlambiti, ameishukuru Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Uwanja wa Taifa kwa kuwapa cheti cha pongeza kwa kutambua thamani na kazi zinazofanywa na Jumuiya hiyo.
Mlambiti, amewataka wana Jumuiya kushikamana na kuwa kitu kimoja katika kuijenga Jumuiya na kutangaza kazi zinazofanywa na Mhe. Rais pamoja na Chama Cha Mapinduzi katika kusimamia Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Post a Comment