DC NSEMWA AWATAKA VIONGOZI NA JAMII KUSHIRIKIANA KUKEMEA UKATILI WA KIJINSIA.
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amewataka Viongozi kwa kushirikiana na Jamii kupinga na kukemea kwa nguvu zote vitendo vya ukatili wa watoto na wanawake ambavyo vinaonekana kukithiri.
Ametoa rai hiyo Februari 20, 2023 katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la kupitisha mpango na Bajeti ya Manispaa ya mwaka wa fedha 2023/2024.
DC Nsemwa, amesema kesi za vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake ni vingi hivyo amewataka viongozi na wananchi kupinga na kuvikemea vitendo hivyo kwa nguvu zote.
ameongeza kuwa inasikitisha kuona vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake vinafanywa na watu wenye akili timamu na wanaojua madhara yake.
"Mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili vinaweza kukomeshwa endapo sisi viongozi tukishirikiana kikamlifu na jamii, kwa sababu chanzo cha vitendo hivyo ni familia, wazazi na walezi, ndiyo maana vitendo hivyo hufanyika majumbani na wanaofanya ni ndugu wa karibu. "Amesema DC Nsemwa.
Hata hivyo, DC Nsemwa, amesema kuwa ukatili unasababishwa na mambo kama ulevi, mila na desturi, mfumo dume na kutoheshimu haki za watoto.
"Hatuawezi kuwa na ulinzi na usalama wa kutosha kwa wanawake na watoto endapo wataendeleza vitendo hivi vya kikatili kwa sababu ukatili huu unafanyika kwa kificho hivyo ulinzi kwa wanawake na watoto unakuwa mdogo kwa sababu hawajitokezi kuleta malalamiko hayo," Ameongeza DC Nsemwa.
Katika hatua nyingine, amewaasa wazazi kuwa makini na watoto ikiwa ni pamoja na kuwaonesha tamthilia ambazo zinalenga mmomonyoko wa maadili, pia amemuomba Mkurugenzi kuandaa semina ya Madiwani na watendaji wa Kata ili kujadili vitendo vya ukatili ya kupata njia sahihi ya kukomesha vitendo hivyo.
Post a Comment