MEYA KIHANGA AKUNWA NA UTENDAJI KAZI WA WATAALAMU MANISPAA YA MOROGORO.
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Wataalamu wa Manispaa ya Morogoro katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Kauli hiyo, ameitoa katika kikao cha Kawaida cha
Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya
Manispaa Februari 08/2023.
Akizungumza katika Baraza hilo, Mhe. Kihanga,
amesema miradi inayotekelezwa na Manispaa kupitia wataalamu ni mizuri na
imeonesha na kuzingatia thamani ya fedha.
“Wataalumu wetu wanafanya kazi kubwa, tuwapongeze,
miradi inakwenda vizuri, tumeona madarasa ya Pochi la Mama yamekamilika kwa
wakati na watoto wetu wanasoma vizuri, endeleeni kuchapa kazi, tuna ndoto ya
kuwa Jiji, bila kuwa na miradi ya uhakikka ndoto yetu itachelewa kutimia”
Amesema Kihanga.
Katika hatua nyengine, amewataka Madiwani katika
kuelekea Bajaeti ya fedha ya mwaka 2023/2024, wajipange vizuri na kutafakari
kubuni miradi mikubwa ambayo itaongeza mapato ya Halmashauri.
“ Mwaka 2015/2020 Baraza la Madiwani lilifanya
kazi kubwa ya kuibua vyanzo vikubwa vya mapato hadi tunafikisha makusanyo ya
Bilioni 12 sio kazi ndogo, ni kazi yetu
sisi tuliopo tuhakikishe tunabuni vyanzo vipya na vikubwa vitakavyo
tuhakikishia makusanyo makubwa ya mapato , muda mnao Madiwani mjipange kuja na
mikakati mikubwa tunapoelekea Bajeti ya fedha ya mwaka 2023/2024” Ameongeza Mhe.
Kihanga.
Mwisho,amewashukuru Wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuendelea na moyo wa ujenzi wa Taifa kwa kuchangia michango mbalimbali ya Maendeleo, hususani katika Ujenzi wa Maboma ya Shule .
Post a Comment