WADAU NA WAJUMBE WA KAMATI ZA USHAURI WILAYA YA MOROGORO WATAKIWA KUISHAURI SERIKALI KUFANIKISHA MIRADI YA MAENDELEO
KAIMU Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Ruth John, amewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kuishauri Serikali katika kufanikisha miradi ya Maendeleo.
Hayo ameyasema , Februari 10/2023 katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Morogoro (DCC) kilichofanyika Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Kuu Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza wakati wa kuongoza kikao hicho, Ruth, ambaye pia amekaimu nafasi ya Mwenyekiti wa kamati ya ushauri (DCC), amewataka wadau pamoja na wajumbe wote wa kamati ya Ushauri Wilaya kuendelea kuishauri serikali namna gani ya kuboresha utendaji wa kazi na kuleta maendeleo.
"Ninawaomba wajumbe wote wa kamati hii kuishauri serikali bila kuogopa kwani ushauri wenu ni tija kwa maendeleo ya wilaya yetu" Amesema Ruth.
Aidha, amesema kuwa lengo la kamati ya ushauri Wilaya ni kuhakikisha Wilaya na Halmashauri zinasonga mbele, hivyo wajumbe wasichoke na wawe huru kutoa mapendekezo yao kwa kuchangia mambo mbali mbali kwa mustakabali wa maendeleo ya Wilaya.
"Lengo la kamati ya ushauri ni kuishauri serikali , sisi tupo tukiwa Viongozi wa Wilaya tukisimamia Maendeleo, ili kuhakikisha Wilaya yetu na Halmashauri zetu zinasonga mbele kimaendeleo, siyo kwamba yote tunayoyafanya ni sahihi, na ndio maana lengo la kikao ni kutushauri namna gani ya kuboresha utendaji wetu ili kuleta maendeleo makubwa katika Wilaya na Halmashauri zetu " Ameongeza Ruth.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kusimamia vyema mapendekezo ya kamati ya ushauri.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoroo, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka Wajumbe wa kamati ya ushauri kuzungumzia changamoto na kutoa ushauri kwa uhuru ili yatokanayo yaweze kufanyiwa kazi.
"Pongezi kwa watendaji wote kwa kushirikiana kwa pamoja, hayo yote tunayoyafanya ni kutokana na ushauri wenu, na leo pia Ushauri wenu tumeupokea na tutaufanyia kazi kama tunavyochukua siku zingine, na kama mnaona jambo haliendi sawa ni ruksa kwenu kutoa ushauri kwa uhuru kabisa na sisi tutaupokea"Amesema Mhe, Kihanga.
Katibu wa Mkutano huo Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Jeremia Lubeleje, amesema ushauri wa wadau wameupokea na wataenda kuuifanyia kazi ili waweze kupitisha Bajeti nzuri ambayo itakuwa Mkombozi wa Wananchi wa Manispaa ya Morogoro .
" Tumepokea ushauri lakini kwa sasa vipo vipaumbele ambavyo kama Halmashauri tutakwenda navyo katika mwaka wa fedha 2023/2024, hivyo maoni ya wajumbe tumeyapokea na tunakwenda kuyafanyia kazi, lengo letu ni kutatua changamoto za wananchi, kubwa zaidi bajeti yetu ya mwaka 2023/2024 tumeweka kipaumbele zaidi katika kutatua changamoto ya Madawati kwa shule zetu za Msingi pamoja na vipaumbele vyengine" Amesema Lubeleje.
Post a Comment