WICOF WAFANYA KONGAMANO KUBWA MJADALA WA MALEZI, FAMILIA ZAKUMBUSHWA KUZINGATIA WAJIBU WA MALEZI KWA WATOTO.
AFISA Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Faraja Maduhu, ametoa wito wa kuwakumbusha Wazazi kutambua malezi bora kwa watoto kwa faida ya vizazi vijavyo.
Kauli hiyo ameitoa, katika Kongamano la Mjadala wa Familia ,kongamano lililoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la WICOF Chini ya Mkurugenzi wake Mwajabu Dhahabu katika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro Februari 25/2023.
Maduhu,amesema kuwa wingi wa watoto waishio katika mazingira magumu umechangiwa na kuyumba kwa misingi ya malezi bora.
"Watoto wana haki zote ikiwemo kusikilizwa,kusomeshwa na kupendwa,sasa unamkuta mzazi hana muda na watoto matokeo yake wanaishia mitaani"Amesema Maduhu.
" Hakuna mzazi ambaye angependa hatima ya mwanaye iwe ya misukosuko lakini ni vyema kuangalia malezi wanayowapa watoto" Ameongeza Maduhu.
Aidha, Maduhu, amesema Asasi zisizo za Kiserikali wamekuwa wakitoa ushirikiano mzuri na Serikali katika kupunguza wingi wa Watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kutoa elimu na kugharamia Miradi mbalimbali
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Salum Kipira, amesema kama wazazi ndani ya familia hawaheshimiani, hawatoi picha ya thamani ya kuheshimiwa, vivyo hivyo watoto nao watakuwa na ujasiri wa kutoheshimu.
Naye Mkurugenzi wa WICOF , Mwajabu Dhahabu, amesema mzazi ana nafasi ya pekee katika kumwandalia mtoto hatima ya maisha na ni mtu anayemtunza, kumhudumia na kumfundisha mtoto mpaka akue na anaweza kumwambukiza tabia njema au mbaya.
"Si kitendo kibaya mtoto kujibizana na mzazi kwa kuwa kinampa mtoto mawanda mapana ya kuhoji kile ambacho hajaridhia kukitenda, tatizo ni pale linapokuja suala ambalo linahitaji nafasi ya mzazi ijidhihirishe kwa mtoto, lakini kwa kuwa mtoto amepewa uhuru uliopitiliza na mazoea yasiyokidhi viwango, anajiinua na kutaka kuififisha nafasi ya mzazi" Amesema Mwajabu.
Katika Kongamano hilo la Mjadala wa familia, vilendana sambamba na zoezi la uchangiaji wa damu pamoja na maonesho ya bidhaa za wajasiriamali.
Post a Comment