Header Ads

Kutoka benki ya Dunia & Esmap, “Mkopo na msaada Trilioni 1.333



Tanzania na Benki ya Dunia zimetiliana saini mikataba miwili ya mkopo nafuu na msaada yenye thamani ya dola za Marekani milioni 579.93 sawa na Tsh. Trilioni 1.333, kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ukiwemo mradi wa maji safi na usafi wa mazingira pamoja na mradi wa kuboresha afya ya Mama na Mtoto.

Waliotia saini mikataba hiyo Jijini Dar es salaam, ni Waziri wa Fedha na Mpango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.

Dkt. Nchemba amesema kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 550 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.264 ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 29.93 sawa na shilingi bilioni 68.79 ni msaada kutoka Energy Sector Management Assistance Program (ESMAP) na Mfuko wa Global Financing Facility.

Dkt. Nchemba amefafanua kuwa Mradi wa Mpango Endelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira umetengewa dola za Marekani milioni 300 (bilioni 689.51) ambazo ni mkopo wenye masharti nafuu kupitia dirisha la IDA na dola milioni 4.93 ambazo ni msaada huku Mradi wa kuboresha Afya ya Mama na Mtoto ukipewa dola za Marekani milioni 250 (bilioni 574.59) na msaada wa dola za Marekani milioni 25 sawa na shilingi bilioni 57.46.

“Miradi iliyopewa fedha inaendana na malengo ya Taifa ya kuboresha Maisha ya watu kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 hadi 2025/2026, na Dira ya Zanzibar ya 2050, ikiwa ni ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuongeza upatikanaji wa maji vijijini na mijini na uboreshaji wa mazingira na utoaji wa huduma bora za afya na za uhakika za Mama na Mtoto, Tanzania Bara na Zanzibar”

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.