MILIONI 400 ZATENGWA KUFUNGUA BARABARA ZA MITAA MANISPAA YA MOROGORO.
MANISPAA ya Morogoro imepanga kutumia jumla ya shilingi milioni 400 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kufungua barabara za mitaa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, wakati akijibu swali kuhusu ni lini Manispaa itaboresha barabara , swali lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Mindu, Mhe. Zuberi Mkalaboko katika Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Madiwani uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Kuu Manispaa Februari 08/2023.
Akizungumza kuhusu kero za barabara, Machela, amesema changamoto ya barabara ni Manispaa yote hivyo kama Halmashauri tayari imeshatenga fedha hizo ili kuhakikisha inafungua barabara na wananchi wapate huduma ya usafiri.
" Tumeona tutenge hizi fedha, nipongeze Baraza la Madiwani kwa kukubali kutenga fedha hizi, changamoto ni kubwa ya barabara zetu, tukisema tusubirie TARURA , bado tunaoana wenzetu bajeti yao sio kubwa ya kukidhi matakwa yetu, tunaamini kupitia fedha hizi tutafungua barabara na tutakuwa kwa kiasi fulani tumetatua changamoto hii ambayo imekuwa ikitusumbua sana " Amesema Machela.
Machela, amesema kuwa katika Bajeti ya mwaka 2022/2023 , Manispaa ilitenga fedha ya ununuzi wa Greda la kuchonga barabara lakini bajeti hiyo haikupita hivyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 watatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa greda .
" Tumeshapata idhini ya kununua Greda kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa, tunaamini katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, tunakwenda kutenga bajeti ili tununue greda letu na kutatua changamoto za barabara na hii itasaidia miji yetu kukua kwa kasi, maana watu watajenga nyumba na huduma za kijamii zitasogea ikiwa ni pamoja na magari ya usafiri kuweza kufika eneo kwa uhakika tofauti na ilivyo kwa sasa " Ameongeza Machela.
Post a Comment