Header Ads

BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA MOROGORO YAIDHINISHA SHILINGI BILIONI 95.6 MWAKA WA FEDHA 2023/2024.




BARAZA la Madiwani Manispaa ya Morogoro imeidhinisha  kutumia kiasi cha shilingi 95.690,984,212.00  katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga katika  Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la kupitisha mpango na Bajeti ya Manispaa ya Mwaka 2023/2024.

Akizungumza katika Baraza hilo, Mhe. Kihanga, amesema , matumizi  hayo yamepanda kwa asilimia 13.16 ya matumizi  ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo mwaka wa 2022/2023 Manispaa ilitumia kiasi cha shilingi 87,256,281,250.00.

Mhe. Kihanga ,amesema kuwa ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa fedha za mishahara ya ajira mpya na promosheni ya watumishi ambapo mishahara ni Bilioni 72,071,194,000.00, matumizi mengineyo Bilioni 1, 152,173,000.00, miradi ya maendeleo shilingi  Bilioni 9,639,944,669.00, na Shilingi Bilioni 12,813,917,512.00 ya mapato ya ndani.

Miongoni mwa vipaumbele vya bajeti ya mwaka  2023/2024 ambavyo Mhe. Kihanga amevitaja ni pamoja na Kumalizia tatizo la madawati sekta ya elimu Msingi na Sekondari, kuhamisha machinjio ya Manispaa kwenda Kata ya Mkundi, kumalizia miradi viporo ndani ya Manispaa ikiwamo Ofisi za Kata na Mitaa, Kuanzisha ujenzi wa Ofisi Mpya ya Manispaa kuijenga Kihonda (SGR), Kuanzisha ujenzi wa  Ukumbi mkubwa na Hotel katika eneo la Gymkhana, kumalizia maboma 50 ya madarasa ya kiushindani shule za msingi , kufungua barabara mpya na kukabidhi TARURA ndani ya Manispaa kwa kununua Greda, kuanzisha mradi wa kununua , kufidia na kuuza viwanja , Ujenzi wa Vyumba 2 vya upasuaji Vituo vya Afya Mafiga na Sabasaba, kumalizia miundombinu ya Zahanati ya SINA, Kufanya ukarabati Zahanati ya Mji Mpya, kumalizia ujenzi Kituo cha afya Tungi, Kumalizia na kuongeza miundombinu ya shule ya Sekondari ya Ghorofa Boma, kumalizia majengo ya elimu ya sekondari ya Lukobe na Mindu, Utoaji wa mikopo asilimia 10 kwa makundi maalum Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu pamoja na kuboresha miundmbinu ya machinga na vitega uchumi vya manispaa kwa lengo la kuongeza mapato.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro,Mhe. Rebeca Nsemwa,  amesema mapendekezo ya Bajeti yamelenga kutatua changamoto za wananchi pamoja na kufanikisha ndoto ya Manispaa kuwa Jiji.

DC Nsemwa, amewataka Madiwani pamoja na watumishi wa Manispaa ya Morogoro kuwa kitu kimoja ili kuweza kufanikisha kwa ufanisi bajeti ambayo inakwenda kupitishwa ya mwaka 2023/2024.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amewaambia Madiwani waendelee kuwaamini wataalamu  huku akiwaahidi kuitekeleza Bajeti hiyo na kuifanya ndoto ya Manispaa kuwa Jiji inakamilika.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.