Man Utd 1-2 Sevilla: Jose Mourinho asema klabu hiyo kuondolewa UEFA si jambo geni
Meneja wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho amesema hatua ya klabu hiyo kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika hatua ya 16 bora "si jambo geni" kwa klabu hiyo na si mwisho wa dunia.
Manchester United walilazwa 2-1 na Sevilla uwanjani Old Trafford, mabao yote ya klabu hiyo ya Uhispania yakifungwa na nguvu mpya Wissam Ben Yedder.
"Sifikirii uchezaji wetu ulikuwa mbaya," alisema Mourinho baada ya mechi hiyo ambayo ilikuwa mara ya nne kwake kushindwa katika hatua hiyo ya muondoano Ulaya.
Aliongeza: "Sina majuto. Nilifanya kazi kadiri ya uwezo wangu, wachezaji walijitolea pia. Tulijaribu sana, tulishindwa na hiyo ndiyo kawaida ya mchezo huu wa soka."
United walionekana kuzidiwa na klabu hiyo ya Uhispania mechi zote mbili na Mourinho aliadhibiwa kutokana na timu yake kuwa na tahadhari zaidi katika mechi hiyo ya marudiano Jumanne.
United walipoteza nafasi ya kujiunga na wapinzani wao wa jiji Manchester City na Liverpool ambao tayari wamefuzu kwa robo fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mashetani hao wekundu sasa wameshinda mechi moja pekee kati ya tisa walizocheza hatua ya muondoano katika mashindano ya Ulaya na wametolewa kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika hatua sawa katika misimu miwili kati ya mitatu waliyocheza karibuni, awali ikiwa 2012-13 na 2017-18.
United walikuwa wameanza kwa matumaini ambapo katika dakika tano za kwanza Romelu Lukaku alipata fursa ya kumfanyisha kipa wa Sevilla kazi ya ziada, lakini walianza kuzidiwa nguvu baada ya hapo.
Mourinho alisema: "Niliketi kwenye kiti hiki mara mbili katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kuwaondoa Manchester United [katiak hatua ya 16 bora] wakiwa kwao nyumbani, Old Trafford. Katika kiti hiki nikiwa na Porto (mwaka 2004) na Real Madrid (mwaka 2013), waliondolewa mara zote mbili. Si jambo geni kwa klabu hii.
"Sifikirii uchezaji wetu ulikuwa mbaya sana, nafikiri nia yetu na jinsi tulivyoanza mechi ilikuwa nzuri na ya matumaini. Sevilla ni timu nzuri na wanaweza kuuficha mpira na wana wachezaji ambao ni wazuri sana katika hilo safu ya kati. Walifanya hivyo kipindi kirefu cha mechi.
"Nafikiri bao la kwanza kawaida lingekuwa muhimu sana, sio tu kwa sababu ya matokeo ya mkondo wa kwanza lakini pia kwa sababu ya umuhimu wa mechi yenyewe.
"Wakati mwingine huwa nabahatika na mabadiliko ninayoyafanya kwenye kikosi, wakati mwingine unakuta mameneja wengine ndio wanaobahatika. Ilikuwa vyema, na hatua nzuri kwa Vincenzo kumuingiza uwanjani Ben Yedder (aliyefunga bao). Walipofunga bao la kwanza, mechi ilibadilika kabisa."
Sevilla ndiyo klabu ya tatu pekee kufunga mabao mawili au zaidi Old Trafford dhidi ya United uchini ya ukufunzi wa Mourinho (Manchester City mara mbili na Burnley).
City ndiyo klabu nyingine pekee iliyofanikiwa kuwalaza United Old Trafford chini ya Mourinho (1-2 Septemba 2016 na 1-2 Desemba 2017).
Ikizingatiwa kwamba Manchester City wanaelekea kushinda Ligi ya Premia, United sasa wataangazia Kombe la FA katika tumaini lao la pekee kushinda kikombe msimu huu.
Watakutana na Brighton katika raundi ya sita Jumamosi.
Post a Comment