Atiwa mbaroni kwa tuhuma za kumchinja mkewe
Jeshi la Polisi Mkoani Katavi inamshikilia mwanamume mwenye umri wa miaka 45, akituhumiwa kumuua mkewe kwa kumchinja kisha kuchimba shimo na kufukia mwili.
Inadaiwa kuwa mwanamume huyo, mkazi wa Kijiji cha Songambele Kata ya Simbwesa mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Tanganyika Mkoa wa Katavi, alitenda unyama huo miezi mitatu iliyopita huku mwanawe mdogo wa miaka mitano akishuhudia.
Inadaiwa alifanya hivyo, akimtuhumu mkewe mwenye umri wa miaka 31 kuwa ni malaya aliyekubuhu. Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Damas Nyanda hakuwa tayari kutaja majina ya mtuhumiwa huyo, akidai ni kwa sababu za upelelezi wa kipolisi.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda Nyanda alisema mwili wa marehemu huyo, uligundulika saa sita mchana juzi katika Kijiji cha Songambele ukiwa umefukiwa shimoni, baada ya kufukiwa miezi mitatu iliyopita.
“Upelelezi wa awali wa kipolisi umebaini kuwa marehemu huyo aliuawa na kufukiwa shimoni humo Januari 15, mwaka huu, baada ya kushambuliwa na mumewe kwa kupigwa na mpini wa jembe na kucharazwa viboko kisha akamnyonga.
“Mume alikuwa akimtuhumu mkewe huyo kuwa ni malaya aliyekubuhu na wakati akimfanyia ukatili huo mkewe, mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka mitano alikuwa katika eneo hilo la tukio akishuhudia kila kitu kilichofanyika,” amesema Kamanda Nyanda.
Inadaiwa kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, mwanamume huyo alirejea nyumbani na kuendelea na maisha yake kama kawaida, huku akimtishia mara kwa mara mtoto wake kuwa akivujisha siri hiyo, atakiona cha mtema kuni. Pia alimuelekeza kuwa akiulizwa, aseme kuwa mama yake amesafiri.
Amesema jeshi la polisi lilimtia nguvuni mwanamume huyo juzi na baada ya mahojiano alikiri kufanya mauaji hayo na alikuwa tayari kwenda kuwaonesha polisi alipomfukia mkewe.
Aliwaongoza polisi katika eneo la tukio ambapo alifukua udongo na mwili wa mkewe ulikutwa ukiwa umeshaharibika, na kwa sasa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, mjini Mpanda.
Post a Comment