Header Ads

Trump kuitoza Rwanda ushuru wa nguo zake zinaoagizwa na Marekani, Tanzania na Kenya zanusurika

Rais Donald Trump
Image captionRais Trump amesema kuwa kupiga marufuku mitumba Rwanda imevunja makubaliano ya kibisahara na Marekani chini ya AGOA
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa ataahirisha mpango wa kuiondolea Rwanda ushuru wa nguo zake zinazonunuliwa na Marekani kutoka Rwanda.
Bw Trump hata hivyo amesema Tanzania, Uganda na Kenya hazitachukuliwa hatua
Uamuzi huo wa Trump wa kuiwekea Rwanda ushuru wa nguo zake katika soko la Marekani umetokana na Rwanda kuweka vikwazo kwa nguo na viatu vya mitumba vinavyotoka Marekani.
Rais Trump amesema kuwa kupiga marufuku mitumba Rwanda imevunja makubaliano ya kibiashara na Marekani chini ya AGOA.
Soko la mitumba nchini Uganda
Image captionSoko la nguo za mitumba na wanunuzi nchini Uganda. Biashara hii imeshamiri katoka nchi za Africa Mashariki
Wafanyabiashara wa nguo za mitumba nchini Marekani wanadai kuwa mpango wa mataifa ya Rwanda, Tanzania na Uganda wa kupiga marufuku nguo na viatu vya mitumba unaathiri sekta yao.
Muungano wa wafanyabiashara wa bidhaa zilizotumiwa (SMART), maarufu kama mitumba unakadiria kuwa kazi 40,000 za Wamarekani zinazohusiana na ukusanyaji, utengenezaji na uuzaji wa nguo za mitumba zitaathirika iwapo nchi za Afrika Mashariki za Rwanda, Tanzania na Uganda zitatekeleza mpango wake wa kupiga marufuku nguo na viatu vya mitumba kama zilivyokubaliana.
Chini ya mkataba wa ushirikiano wa kibiashara baina ya Afrika na Marekani (AGOA) baadhi ya nchi za Afrika Rwanda ikiwemo ziliondolewa ushuru wa baadhi ya bidhaa zake zinazouzwa Marekani.
"Hata hivyo Marekani inaendelea kutoa faida za AGOA kwa mataifa ya Tanzania na Uganda kwa sababu nchi hizo zimechukua hatua ya kuondoa kodi ya nguo na viatu vya mitumba na kuamua kutopiga marufuku bidhaa hizo," alisema mwwakilishi wa ofisi ya biashara ya Marekani.
Biashara ya mitumba
Image captionBiashara ya mitumba imekuwa chanzo cha kipato kwa wafanyabiashara wengi Afrika Mashariki
"Ninaipongeza Tanzania na Uganda kwa kuchukua hatua za kupatia suluhu hofu za Marekani," afisa wa masuala ya biashara katika ofisi rais nchini Marekani C. J. Mahoney katika taarifa yake.
"Tumekuwa na tutaendelea kushirikiana na Rwanda kutatua tatizo hili."
Kenya pia imetajwa kama taifa ambalo linachukua hatua.
Katika barua yake kwa Baraza la Congress, Trump amesema muda wa Rwanda kuuza bidhaa zake bila ushuru nchini Marekani utamalizika katika 60 kama Rwanda haitarekebisha maamuzi ya hatua ilizochukua.
Mpango wa AGOA hutoa huziwezesha nchi zilizo chini ya jangwa la sahara kuingiza Marekani bidhaa zake ambazo zimetimiza masharti fulani yaliyokubaliwa, ikiwemo kuondoa vikwazo kwa biashara za Marekani na uwekezaji miongoni mwa mengine.

Ushirikiano wa Rwanda na Marekani kibiashara:

Mkataba wa ushirikiano wa kibiashara baina ya Marekani na Rwanda (BIT) chini ya mkataba wa AGOA ulisainiwa Januari 2012, lakini yakazinduliwa rasmi 2007.
Rwanda ni mshirika wa 165 wa biashara wa Marekani kwa ukubwa wa bidhaa zinazouzwa baina ya nchi mbili kulingana na takwimu za 2016.
Bidhaa zinazouzwa na Marekani kwa Rwanda zilifikia milioni $75; na zilizoingizwa Marekani kutoka Rwanda zilikuwa za jumla ya dola milioni $26 milioni.
Mauzo makuu ya Rwanda kwa Marekani ni yale yatokanayo na kilimo kama Kahawa, Chai, karanga, matunda na mboga za kusindikwa pamoja na nguo.
Kwa upande wake Marekani huiuzia Rwanda : ndege za safari, mashine za kielektroniki, zana za tiba na dawa.
Baadhi ya Mataifa ya Afrika Mashariki yaliazimia kupiga marufuku uagizwaji wa nguo za mitumba ili kuboresha sekta ya viwanda vya nguo katika nchi zao.
Hata hivyo wakosoaji wa marufuku hiyo wanadai bado sekta ya viwanda vya nguo katika nchi hizo haijaimarika kiasi cha kuzalisha nguo za kutosha kwa wakazi wa nchi hizo na kuweza kuuza bidhaa hiyo nchi za nje.
Wanadai pia kuwa kupigwa marufuku kwa bidhaa za mitumba kutachangia ukosefu mkubwa wa ajira kwa wafanyabiashara wanaotegemea uuzaji wa nguo hizo kwa ajili ya kipato chao.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.