Mtibwa Sugar yawatembezea kipigo Watoto wa Julio
TIMU ya Mtibwa Sugar leo imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma FC katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Mabao ya Mtibwa Sugar inayofundishwa na kocha mzalendo, Zuberi Katwila ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo yamefungwa na Haroun Chanongo na Salum Kihimbwa yote kipindi cha kwanza.
Pamoja na kufungwa, Dodoma FC ya Daraja la Kwanza Tanzania Bara inayofundishwa na kocha nguli nchini, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ilicheza vizuri, tu ilishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza huku ikiwaruhsu wageni kupata mabao ya mapema.
Kwa Mtibwa Sugar, mchezo huo ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wake wa Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya wenyeji, Azam FC Machi 31 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Robo Fainali za Azam Sports Federation Cup zitaanza Machi 30, Stand United wakiikaribisha Njombe Mji FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na mbali na Azam FC kuwa wenyeji wa Mtibwa kuanzia Saa 2:00 usiku Machi 31, Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Aprili 1, Uwanja wa Namfua mjini Singida, Yanga watakuwa wageni wa Singida United.
Post a Comment